Na mwandishi wetu
Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya leo Jumatano amefanikiwa kuibuka kidedea kwa kuwa mfungaji wa bao bora la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi msimu huu.
Mudathir ameibuka mshindi akiwabwaga Aymen Mahous wa USM Alger alipoifunga FC Lupopo, Aubin Kramo wa Asec Mimosas alipoinyoosha Diables Noirs na Paul Acquah wa Rivers United dhidi ya DC Motema Pembe.
Mchezaji huyo ameshinda kupitia bao lake alilowafunga TP Mazembe kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam katika ushindi wa mabao 3-1 walioupata Yanga katika mechi hiyo.
Kiungo huyo amewaangusha wapinzani wake kwa kura asilimia 70 dhidi ya Aymen mwenye asilimia 21, Kouame asilimia 5 na mwisho ni Acquah aliyeambualia asilimia tatu.
Kura hizo zilianza kupigwa juzi na mashabiki kupitia ukurasa wa mtandao wa Twitter wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wa michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Mudathir na Farid Mussa ambao wote wamewahi kukipiga Azam ndio wachezaji pekee wazawa wa Yanga waliofunga mabao katika hatua hiyo ambapo Yanga imefunga jumla ya mabao tisa na kufungwa manne.
Mabao mengine saba ya Yanga yamefungwa na Fiston Mayele, Tuisila Kisinda, Kennedy Musonda na Jesus Moloko ambao wote ni wachezaji wa kigeni.
Kwenye Ligi ya Mabingwa bao la Mahmoud Karhaba wa Al Ahly alilowafunga Al Hilal ndio limekuwa kinara dhidi ya mengine yaliyofungwa na Hamdou El Houni wa Esperance dhidi ya CR Belouizdad, Makabi Lilepo wa Al Hilal alipoichapa Coton Sport na Teboho Mokoena wa Mamelodi Sundowns walipocheza na Al Ahly.
Kimataifa Mudathir kinara bao bora CAF
Mudathir kinara bao bora CAF
Read also