Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake katika mechi iliyokuwa ngumu dhidi ya African Sports ambayo hata hivyo timu yake ilipata ushindi wa mabao 4-0.
Kwa ushindi huo uliopatikana jana Alhamisi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Simba hatimaye imefanikiwa kukata tiketi ya robo fainali ya michuano ya Kombe la FA (ASFC).
Mgunda alisema wapinzani wao waliwapa wakati mgumu dakika takriban 30 za awali kutokana na kutowafahamu kiufundi lakini baadaye waliwasoma na kuwazidi kete.
“Tumepata matokeo mazuri lakini tukiri tulikuwa tunacheza na timu ambayo hatujui kiufundi wakoje ndio maana dakika 20 mpaka 25 za kwanza ilikuwa tabu lakini tuliwasoma humohumo na tukawapatia majibu humohumo ndio maana kipindi cha pili mechi ikawa nyepesi kidogo,” alisema Mgunda.
“Lakini pia tuliwaheshimu Sports japo wapo daraja la chini lakini hizi ni mechi za mtoano, hata vijana tuliowapa nafasi ambao hawaonekani kwenye mechi nyingine wamefanya vizuri na sisi tumejifunza kitu kutoka kwao na wao wamejifunza kitu kwenye mechi za kimashindano kama hizi,” alisema Mgunda.
Naye Kocha Mkuu wa Sports, Omari Mussa alisema walianza vizuri kwa mbinu za kuwabana Simba lakini baadaye kipa wao alifanya makosa ya kiufundi na kufungwa bao la kwanza lililowatoa mchezoni wachezaji wake.
“Goli la kwanza ilikuwa muda wote tunacheza kama kipa ndiyo mlinzi wa mwisho lakini alichelewa kidogo na tukafungwa, tukazungumza na vijana kuelekea kipindi cha pili lakini ikawa kama wametoka mchezoni na mwisho tukaruhusu mabao rahisi sana.
“Lakini nimeridhika na kiwango kilichooneshwa ukizingatia tumecheza na timu kubwa, ina wachezaji wazoefu ila kuna kitu tumekipata ambacho kitatusaidia tukirejea kwenye mechi za Championship maana huko pia hatuko vizuri kwa hiyo hii mechi itatusaidia,” alisema Mussa.