Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Rivers United ya Nigeria ili kuwemo katika rekodi ya walioshuhudia timu hiyo ikipenya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji amesema leo Jumatano kuwa kuna uwezekano mkubwa msimu huu wakapata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye nusu fainali hiyo hivyo licha ya mashabiki kujitokeza kuiunga mkono timu lakini pia kuwemo kwenye historia hiyo.
Yanga itaumana na Rivers Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ikiwa tayari na faida ya ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa awali uliopigwa Uyo, Nigeria wikiendi iliyopita.
Na kwenye mechi hiyo ya marejeano, Rivers inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 3-0 ili kusonga mbele wakati Yanga ikihitaji sare pekee kutinga nusu fainali.
“Kuna uwezekano mkubwa sana nchi ikapata mwakilishi wa nusu fainali katika michuano ya Kombe la Shirikisho, ni jambo kubwa kwa nchi, basi Wananchi nao wajitokeze kwa wingi kuhakikisha wanakuwa sehemu ya historia ya siku ya tarehe 30.
“Miaka kadhaa mbele mtu aweze kusema kwamba siku timu imekwenda hatua ya nusu fainali na mimi nilikuwepo kuishangilia lakini pia wajitokeze kuendelea kuwapa hamasa wachezaji wetu kuonesha kwamba tuko pamoja nao katika kuipambania timu,” alisema Haji.
Pamoja na hayo, Haji alisisitiza kuelekea mechi hiyo uongozi mzima pamoja na benchi la ufundi wamekubaliana kwamba bado hawajamaliza mechi ya robo fainali kwani wanazitegemea dakika 90 nyingine za mechi ya Jumapili hii kujihakikishia hilo, hivyo hawatabweteka.
“Unajua mechi hizi ni dakika 180, tushamaliza 90 za kwanza na sasa tunahitaji subira na kujipanga upya tena kwa 90 nyingine za pili ambazo ndiyo zitatoa jibu kwa hiyo uongozi, benchi la ufundi tumekubaliana bado hatujapita, tusibweteke na maandalizi yaendelee kama vile huu ndiyo mchezo wa kwanza wa robo,” alisema Haji.
Kuonesha Yanga inaihitaji kucheza hatua hiyo, baada ya juzi kurejea nchini, hawakupumzika ambapo kikosi kimeendelea na kambi ya maandalizi ya mchezo wao huo.