Naples, Italia
Klabu ya Napoli ya Italia hatimaye imebeba taji la Ligi Kuu Italia au Serie A ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 33 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Udinese jana Alhamisi usiku.
Alikuwa ni Victor Osimhen aliyeifungia Napoli bao la kusawazisha lililoihakikishia timu hiyo pointi moja waliyohitaji ili kutangazwa mabingwa wa Seria A msimu wa 2022-23 baada ya kuwa nyuma kwa bao la mapema la Udinese lililofungwa na Sandi Lovric.
Napoli sasa watacheza mechi tano zilizobaki za ligi hiyo kwa raha zao wakiwania kuboresha rekodi za ushindi kwani tayari taji la Serie A lipo kwenye himaya yao na tayari jiji la Naples limeshalipuka kwa shangwe na nderemo za mashabiki tangu jana usiku.
Mara ya mwisho Napoli ilibeba taji la Serie A mwaka 1990 ikiwa na gwiji wa soka duniani na nahodha wa zamani wa Argentina, Diego Maradona baada ya kubeba taji lao la kwanza miaka mitatu kabla.
“Kuwaona watu wa Napoli wakiwa na furaha inatosha kukupa fikra za hali waliyo nayo kwa sasa katika fikra zao,” alisema kocha wa Napoli, Luciano Spalletti.
“Hawa watu watalilikumbuka tukio hili pale maisha yanapokuwa magumu, wana kila sababu ya kushangilia jambo hili, unajiona katika hali ya utulivu kwa kuwapa tukio la furaha ya aina hii,” alisema Spalletti.
Napoli mataji yake ya mwisho yalipatikana wakati za zama za Maradona ambaye pia alikuwa nahodha wa timu ya Taifa ya Argentina na ambaye uwanja wa klabu hiyo umepewe jina lake, mataji hayo yalibebwa mwaka 1987 na 1990.
Baada ya mafanikio hayo, Napoli iliangukia katika majanga ya kiuchumi ikafilisika na kushuka hadi ligi ya chini ya Serie C na ingawa waliwahi kubeba taji la Coppa Italia mara tatu, kiu ya mashabiki wa timu hiyo ilikuwa ni kubeba taji la Serie A, kiu ambayo hatimaye imekatwa rasmi jana usiku huku mashabiki zaidi ya 10,000 wakisafiri kutoka Naples ili kuishuhudia timu hiyo ikibeba taji hilo baada ya sare ya ugenini na wengine wakifurahia wakiwa nyumbani..