Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba inatarajia kuondoka nchini alfajiri kuelekea mjini Conakry, Guinea kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya AC ya nchini humo.
Simba ambayo inaumana na Horoya ukiwa ni mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya ligi hiyo, imeeleza kuwa itaondoka na msafara wa watu 45, wachezaji 25, wengine ni benchi la ufundi na viongozi.
Timu hiyo itapaa na ndege ya Shirika la Ndege ya Ethiopia, ambapo msafara huo utapitia nchini Ethiopia na kubadili ndege wakitarajia kufika Guinea kesho jioni.
Akizungumzia mchezo wao huo utakaopigwa Jumamosi hii saa moja jioni kwenye Uwanja wa Jenerali Conte, kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema wanahitaji kufanya vizuri kwenye mchezo huo na wamejiandaa kufanya hivyo kulingana na maandalizi waliyokuwa nayo.
“Nafurahi kwanza wachezaji wamekuwa wakinielewa mapema jinsi inavyotakiwa, aina ya mifumo na hata falsafa ya kuutaka mpira uchezwe bila kuupiga mbali inaeleweka, naamini tutakwenda kufanya vizuri kulingana na morali na matokeo tunayoyahitaji lakini kubwa maandalizi tuliyokuwa nayo.
“Kwenye mpira chochote kinawezekana na tunahitaji haya matokeo, ukitazama jinsi tunavyocheza kila mchezo inaonesha jinsi gani hata wachezaji wanataka mafanikio kila kaombe wanaloshiriki na sasa tunakwenda kupambana Afrika,” alisema Robertinho.
Alisema licha ya michuano hiyo lakini pia amepanga kuijenga Simba tishio na yenye kupata matokeo mfululizo katika michuano wanayoshiriki lakini kwanza ushindi dhidi ya Horoya ndiyo kitu muhimu zaidi kwa sasa.
Ukiachana na Horoya, timu nyingine zitakazoumana na Simba kutafuta tiketi ya kutinga robo fainali kutoka Kundi C ni Raja Casablanca ya Morocco na Vipers ya Uganda iliyokuwa ikinolewa na Robertinho kabla ya kutua Simba hivi karibuni.
Msimu uliopita Simba iliishia robo fainali ikitolewa na kwa matuta 4-3 na Orlando Pirates ya Afrika Kusini baada ya kila timu kushinda bao 1-0 nyumbani kwake ambapo safari hii Simba inatazamia kuvuka hatua hiyo na kuweka rekodi mpya ya michuano hiyo.
Soka Simba yaifuata Horoya FC
Simba yaifuata Horoya FC
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
