Clara wa Serengeti apania rekodi ya dunia
Na mwandishi wetu
Clara Luvanga, straika wa timu ya Taifa ya wasichana chini ya miaka 17 Serengeti Girls, anaiwakilisha vyema timu hiyo katika kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia akiwa ameifungia mabao 10.
Kwa mabao hayo, Clara anashika nafasi ya pili duniani akiwa ametanguliwa na Rose Maalouf wa Canada mwenye mabao 12 na ambaye timu yake tayari imefuzu fainali hizo lakini Clara ametamba kuwa lengo lake ni kuhakikisha anaweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa dunia.
Akizungumzia dhamira yake hiyo, Clara alisema kwamba kwa sasa timu yao iko kambini Zanzibar ikijiandaa kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Cameroon ambapo amepania kufunga mabao matatu (hat trick) katika mechi hiyo itakayopigwa Juni 5 mwaka huu na hivyo kumzidi Rose.
“Tuko kambini, tunajiandaa kwa mchezo wa mwisho, nitafanya mazoezi kwa bidii ili kiwango changu kiimarike na kuweza kufunga mabao ili niwe namba moja duniani na Afrika,” alisema Clara.
Mchezaji huyo wa Yanga Princess inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Bara, nyota yake katika mabao ilianza kung;ara katika mechi ya raundi ya pili dhidi ya Botswana ambapo alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 7-0 ilioupata Serengeti.
Baada ya mchezo huo wa nyumbani, nyota ya Clara iliendelea kung’ara ugenini alipopiga hat trick wakati Tanzania ikitamba kwa kuichapa Botswana mabao 4-0 na hivyo kupata ushindi wa jumla wa mabao 11-0.
Katika mechi nyingine ya timu hiyo dhidi ya Burundi, Clara alifunga mabao mawili wakati timu yake ikitoka na ushindi wa mabao 4-0 ugenini lakini mambo hayakuwa mazuri katika mechi ya marudiano nyumbani baada ya Tanzania kulala kwa mabao 2-1 na hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2.
Wakati timu hiyo ikisubiri kurudiana na Cameroon kwenye Uwanja wa Amaan, Clara pia anakumbukwa kwa kuondoka na mpira baada ya kufunga mabao matatu katika mechi ya kwanza ugenini ambayo Serengeti Girls ilitoka uwanjani na ushindi wa mabao 4-1.
Ili Cameroon iizuie Serengeti kufuzu fainali hizo za dunia zitakazofanyika nchini India kati ya Oktoba na Novemba mwaka huu, timu hiyo inahitaji ushindi wa mabao zaidi ya matano katika mechi hiyo ya marudiano.
