Madrid, Hispania
Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone amekubali kubeba lawama za mwenendo mbaya wa timu hiyo kwa msimu huu ingawa hakuwa tayari kuthibitisha habari za mshambuliaji wake nyota, Joao Felix kutaka kuondoka katika timu hiyo.
Atletico ambayo jioni hii ya leo Alhamisi inaingia dimbani kuumana ana Elche inashika nafasi ya tano katika La Liga na tayari imetolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushika mkia katika kundi lake na imekosa nafasi ya kushiriki Europa Ligi.
Matatizo ya kifedha yameilazimisha klabu hiyo kumruhusu mshambuliaji wake, Matheus Cunha kuhamia Wolves, wakati ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Miguel Angel Gil Marin aliwahi kusema kwamba Felix anaweza kuondoka katika klabu hiyo iwapo ofa sahihi itatokea.
“Tulikuwa na wachezaji wanne kwenye fainali za Kombe la Dunia (Antoine Griezmann, Angel Correa, Rodrigo de Paul na Nahuel Molina) na wawili kati yao walicheza kwa muda mrefu. Tuna kikosi kizuri labda mtu pekee ambaye hafanyi kile anachotakiwa kufanya ni kocha,” alisema Simeone alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu uwezo wa kikosi chake.
“Kuna wachezaji wazuri, Joao (Felix) alikuwa wa kipekee kwenye Kombe la Dunia, (Yannick) Carrasco na Axel (Witsel) walianza mechi za Ubelgiji, tuna wachezaji muhimu, ni lazima tujiboreshe ili wafikie ubora wa juu kwenye La Liga, tuna msimu mbaya na hilo si suala la majina,” Diego Simeone.
Hadi mechi za La Liga zinasimama kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia, Atletico ilikuwa na ushindi mmoja katika mechi tano na sare mbili kwa Rayo Vallecano na Espanyol na ikapoteza kwa Cadiz na Real Mallorca.
Zipo habari kwamba Simeone hana mahusiano mazuri Joao na hiyo inatajwa kuwa sababu mojawapo ya uwezekano wa mchezaji huyo kuuzwa Januari ingawa kocha huyo anapinga hilo, “Tuna uhusiano mzuri wa kikazi, wakati wote kunaweza kuwapo mambo fulani kati ya watu, hatuwezi kukubaliana kila kitu, lakini tumekuwa tukiangalia mazuri kwa ajili ya klabu.”
