Na mwandishi wetu
Mahasimu wa soka nchini Tanzania, Simba na Yanga wameshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa leo Jumapili Mei 3, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.
Timu hizo zimecheza leo zikiwa zimetoka kucheza mechi ya fainali Kombe la Muungano Jumatano ya Aprili 29, 2026 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar na Simba kuifunga Yanga bao 1-0.
Katika mechi ya leo Simba ndio waliouanza mchezo kwa kasi wakionesha kila dalili za kuendeleza ushindi walioupata Zanzibar.
Kasi hiyo ya Simba ilizaa bao la kwanza mapema dakika ya tatu ya mchezo huo lililofungwa na Libase Guaye kwa shuti la chinichini akiitumia pasi ya Clatous Chama.
Chama aliongeza bao la pili ambalo alilifunga kiufundi katika dakika ya saba baada ya kuinasa pasi ya juu ya kudokoa ya Elly Mpanzu na Chama kubinuka staili ya sarakasi na kuujaza mpira wavuni akimuacha kipa Djigui Diarra asijue la kufanya.
Yanga nao walipambana na kuandika bao lao la kwanza dakika ya 17 lililofungwa na Prince Dube kwa shuti la chini akitumia mpira ulioanzia kwa Maxi Nzengeli.
Nzengeli alipiga pasi ndefu iliyomkuta Duke Abuya akiwa karibu na beki mmoja wa Simba lakini akafanikiwa kumsogezea Dube aliyemalizia kwa kuujaza mpira wavuni.
Dakika tano baada ya kuanza kipindi cha pili, Yanga walipata bao la kusawazisha ambalo lilifungwa na beki wa kati na nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto.
Nyota ya Chama iling’ara mara mbili katika mechi hiyo kwani licha ya bao lake kuwa kivutio kwa namna alivyoonesha ufundi hadi kulifunga pamoja na kutoa pasi iliyozaa bao la kwanza, mchezaji huyo pia ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi hiyo.
Baada ya matokeo hayo Yanga inaendelea kushika usukani wa ligi ikiwa na pointi 48 wakati Simba inabaki nafasi ya pili na pointi 43 huku kila timu ikiwa imecheza mechi 20 hadi sasa.
Kimataifa Yanga, Simba zatoka sare 2-2
Yanga, Simba zatoka sare 2-2
Read also
