London, England
Klabu ya Aston Villa imemkabidhi rasmi Steven Gerrard mikoba ya kuinoa timu hiyo akichukua nafasi ya Dean Smith ambaye ametimuliwa.
Gerrard mchezaji aliyejipatia mafanikio akiwa nahodha wa Liverpool na kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2005, anaachana na timu ya Rangers ya Scotland ambayo ameiwezesha kutwaa taji la Ligi Kuu Scotland akiwa ameinoa timu hiyo kwa miaka mitatu.
Smith alitimuliwa Jumapili iliyopita baada ya Villa kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo hasa vipigo vitano mfululizo huku timu hiyo ikiwa katika nafasi ya 16 kwenye Ligi Kuu England.
Mbali na Liverpool ambayo ameichezea kwa mafanikio akiichezea mechi zaidi ya 700, Gerrard pia alikuwa mchezaji tegemeo wa timu ya Taifa ya England akiichezea zaidi ya mechi 100.
Baada ya kuachana na Liverpool, Gerrard alitimkia nchini Marekani alipojiunga na klabu ya LA Galaxy mwaka 2015 kabla ya kustaafu soka mwaka 2016.
Katika kazi ya ukocha, Gerrard alianzia kwenye timu ya vijana chini ya miaka 18 ya Liverpool alikofanya kazi kwa msimu wa 2017/18.
Kwa kuachana na Rangers, Gerrard amekubali kuanza changamoto mpya kwenye ligi kubwa, ngumu na maarufu ukilinganisha na ile ya Scotland na anainoa timu ambayo mwenendo wake kwenye ligi hiyo hauko vizuri.
Sports Mix Steven Gerrard kocha mpya Aston Villa
Steven Gerrard kocha mpya Aston Villa
Read also
