Na mwandishi wetu
Willy Onana amefufua matumaini ya Simba kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufunga mabao mawili yaliyoipa timu yake ushindi wa 2-0 dhidi ya Wydad.
Ushindi huo uliopatikana leo Jumanne kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam ni wa kwanza kwa Simba katika Kundi B baada ya kupata sare mbili na kupoteza mechi moja dhidi ya Wydad katika mechi tatu za awali.
Baada ya kupoteza matumaini na kukata tamaa Simba sasa ina kila sababu ya kujiamini kwa kufufua matumaini kutokana na ushindi huo kwani umewawezesha kufikisha pointi tano.
Simba sasa wanasubiri kujua matokeo ya mechi nyingine ya kundi lake inayochezwa usiku huu kati ya Jwaneng Galaxy na Asec Mimosa.
Ikicheza bila ya nyota wake wawili waliocheza mechi iliyopita dhidi ya Wydad, Saido Ntibazonkiza na Sadio Kanoute wanaotumikia adhabu, Onana aliandika bao la kwanza dakika ya 35 akiitumia vizuri pasi ya Kibu Dennis.
Dakika tatu baadaye, Onana aliwainua kwa mara nyingine vitini mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao la pili safari hii akiitumia pasi ya Mzamiru Yassin.
Umahiri wa kipa Ayoub Lakred pia uliisaidia Simba kutoka uwanjani na ushindi baada ya kuinyima Waydad nafasi kadhaa ambazo zingeweza kubadili matokeo ya mchezo huo.
Pointi tano ilizofikisha Simba zinaifanya timu hiyo kuishusha Waydad ambayo inabaki na pointi nne na kuburuza mkia katika kundi hilo.
Pamoja na ushindi huo kuiweka Simba katika nafasi nzuri lakini hesabu zinaonesha kwamba bado timu hiyo ina kazi ya kufanya kwani katika mechi mbili zilizobaki timu yoyote katika kundi hilo inaweza kusonga mbele katika hatua ya robo fainali.
Inachotakiwa kufanya Simba kwa sasa ni kuhakikisha inashinda mechi hizo mbili zilizobaki ambazo zitapigwa Februari mwakani, kwanza dhidi ya Asec Memosa jijini Abidjan na mwezi unaofuata dhidi ya Jwaneng, mechi itakayopigwa jijini Dar es Salaam.
Kimataifa Simba yafufua matumaini, yainyoosha Wydad
Simba yafufua matumaini, yainyoosha Wydad
Read also