Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Mohamed Abadallah ‘Bares’ amewapongeza wachezaji wake kutokana na kutangazwa kinara wa tuzo ya kocha bora Mwezi Aprili akisema wao ndiyo waliofanya kazi kubwa.
Bares ametangazwa mshindi wa tuzo hiyo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akiwazidi kocha wa Simba, Roberto Oliveira na Daniel Cadena wa Azam FC.
Alisema matokeo ya uwanjani ndio yamembeba kupewa tuzo hiyo na pia anaamini aliokuwa akichuana nao ni makocha bora na wanafundisha timu kubwa lakini kilichotokea ni ushindi umeamua kuwa upande wake kupitia wachezaji alionao.
“Nishukuru kwa tuzo, niseme imenipa kitu katika kazi yangu, haikuwa rahisi lakini kingine ushirikiano wa timu umesababisha haya, wachezaji wamefanya kazi yao na kupelekea ushindi ulioleta yote haya.
“Kama nilivyosema awali nisijipongeze mwenyewe maana ni suala la timu maana hata makocha niliokuwa nikichuana nao ni makocha wakubwa, bora na wanafundisha timu kubwa pia kwa hiyo nashukuru sana, hii imeongeza kitu kwangu,” alisema Bares.
Bares ametwaa tuzo hiyo ikiwa ni miezi mitatu pekee imepita tangu atue Prisons ambapo mechi zake mbili za mwezi Aprili alizoshinda kwa mabao 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting na Geita Gold zilitosha kumpa tuzo hiyo.
Kocha huyo wa zamani wa JKT Tanzania, alitua Prisons kuchukua mikoba ya Patrick Odhiambo wiki chache baada ya kuipa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi timu ya Mlandege wakiifumua Singida Big Stars kwa mabao 2-1.
Kwa wachezaji tuzo hiyo ya mwezi Aprili ilitua kwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki akiwazidi Jean Baleke wa Simba na Ayoub Lyanga wa Azam.