Istanbul, Uturuki
Mwanasoka wa kimataifa wa Ghana, Christian Atsu amekutwa amekufa baada ya kutokea tetemeko na kuharibu nyumba aliyokuwa akiishi Antakya nchini Uturuki. Chanzo kimoja cha habari kimeeleza.
Atsu mwenye umri wa miaka 31 aliwahi kuzichezea timu za Ligi Kuu England za Everton, Chelsea na Newcastle na hadi umauti unamkuta alikuwa akiichezea klabu ya Ligi Kuu Uturuki ya Hatayaspor.
Atsu alipotea tangu Februari 6 lilipotokea tetemeko la ardhi katika nchi za Syria na Uturuki na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 5000 na majengo makubwa kuanguka ingawa iliwahi kuripotiwa kuwa alipatikana akiwa hai.
“Hatuna maneno ya kuzungumzia huzuni tulio nao, hatutakusahau Atsu, uwe na amani, ulikuwa mtu mzuri,” ilieleza taarifa ya klabu ya Hatayspor kupitia mtandao wa Twitter.
Wakala wa Atsu, Nana Sechere ambaye amekuwa katika mji wa Hatay katika siku za karibuni jana Jumamosi alithibitisha kutokea kwa kifo cha mchezaji huyo kupitia akauni yake ya Twitter.
“Ni kwa masikitiko makubwa nawatangazia watu wote kwamba mwili wa Christian Atsu umepatikana asubuhi hii (Jumamosi)” alisema Sechere.
“Salamu zangu za rambirambi kwa familia na wapendwa wake, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wote waliofanya maombi na kushirikiana nasi,” alisema Sechere.
Atsu alijiunga na Hatayspor, Septembar 2022 baada ya kucheza soka msimu mmoja nchini Saudi Arabia na klabu ya Al-Raed.
Ameichezea timu ya Taifa ya Ghana mechi 65 na mwaka 2015 aliiwezesha timu hiyo kufikia hatua ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kabla ya kupoteza mechi hiyo kwa mikwaju ya penalti mbele ya Ivory Coast ingawa Atsu alitangazwa kuwa nyota wa mashindano hayo.