Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema mchezo ujao wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Azam FC hautakuwa mwepesi kwao hivyo wanajiandaa kwa tahadhari kubwa.
Yanga na Azam wanatarajia kukutana Jumapili hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mechi ya ligi hiyo.
Gamondi alisema kuwa hawawezi kuwabeza wapinzani wao ingawa walishakutana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii mwanzo wa msimu huu na kuwafunga mabao 2-0 hivyo wanafahamiana vizuri.
“Hakuna mchezo mwepesi katika ligi hususan timu zinapocheza na Yanga, kila mmoja hujipanga. Hatuibezi Azam ni timu nzuri na ni timu kubwa, hata ule mchezo tuliocheza Tanga (Uwanja wa Mkwakwani) ulikuwa mgumu sana, tuliona namna walivyokuja hasa kipindi cha pili walionesha mchezo mzuri,” alisema Gamondi.
Alisema kwa kujua ubora wa wapinzani wao wanajiandaa kuhakikisha wanatimiza lengo lao la kuondoka na pointi tatu.
Timu hizo zinakwenda kukutana zote zikiwa kwenye ubora, Azam iko katika nafasi ya pili kwa pointi 13 katika michezo mitano, tofauti ya pointi moja dhidi ya Yanga iliyo nafasi ya tatu kwa pointi 12.
Kinachowatofautisha Azam FC haijapoteza mchezo wowote mpaka sasa ikiwa imeshinda michezo minne na kupata sare moja, huku Yanga ikishinda minne na kupoteza mmoja.