Na mwandishi wetu
Baada ya kuwa katika mapumziko ya miezi miwili, mabingwa watetezi Yanga wamerejea kwenye Ligi Kuu NBC kwa kishindo baada ya kuiadhibu Kagera Sugar mabao 4-0.
Ushindi huo uliopatikana Jumamosi hii, Februari Mosi, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, unaifanya Yanga kushika usukani wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 42.
Yanga walianza kuandika bao la kwanza katika dakika ya 32 mfungaji akiwa ni Clement Mzize aliyefumua shuti kali la mguu wa kulia akiitumia pasi ya Stephane Aziz Ki.
Dakika tano baadaye mambo yaliwaendea kombo Kagera baada ya Yanga kupata penalti ambayo ilitokana na makosa ya Hija Shamte kumuangusha Mudathir Yahya katika eneo la penalti.
Yanga hata hivyo walishindwa kupata bao baada ya mpigaji wa penalti hiyo, Aziz Ki shuti lake kupanguliwa na kipa wa Kagera, Ramadhan Chalamanda na kuzifanya timu ziende mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao moja.
Kipindi cha pili Yanga ilikianza kwa mabadiliko ikimtoa Israel Mwenda na nafasi yake kuingia Pacome Zouzoua, mabadiliko yaliyoonekana kuzidisha mashambulizi kwenye lango la Kagera.
Mashambulizi hayo yalianza kuwapa raha mashabiki wa Yanga katika dakika ya 60 baada ya Mudathir Yahya kufunga bao la pili akiitumia pasi ya Prince Dube.
Pacome alisawazisha makosa ya Aziz Ki kwa kufunga bao la tatu kwa mkwaju wa penalti dakika ya 78, penalti iliyotolewa baada ya Maxi Nzengeli kuchezewa ndivyo sivyo katika eneo la penalti.
Dakika tatu kabla ya kutimia dakika 90, Kennedy Musonda aliipatia Yanga bao la nne na la mwisho kwa kichwa akiitumia pasi ya Maxi Nzengeli baada ya ushirikiano kati yake na Kibwana Shomari.
Yanga ili endeleee kushika usukani wa ligi hiyo italazimika kuiombea mabaya Simba yenye pointi 40 ipoteze au itoke sare mechi yake ya Jumapili dhidi Tabora United.
Soka Yanga yaiadhibu Kagera Sugar 4-0
Yanga yaiadhibu Kagera Sugar 4-0
Read also
