Na mwandishi wetu
Yanga imeendelea kuchanja mbuga katika Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Geita Gold bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Alhamisi hii kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo pia unaifanya Yanga kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 52 katika mechi 19 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 44 katika mechi 20.
Mahasimu wa Yanga, Simba wao wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 42 katika mechi 18 walizocheza hadi sasa.
Bao hilo pekee la ushindi kwa Yanga lilipatikana katika dakika ya 28 ya mchezo huo mfungaji akiwa ni Aziz Ki ambaye sasa anakuwa amefikisha mabao 13 katika ligi hiyo.
Baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Geita, Yanga sasa inajiandaa kwa kibarua kigumu dhidi ya Azam, mechi ambayo itapigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa Jumatatu hii, Coastal Union ikiwa nyumbani Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ilitoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ihefu.
Kwa ushindi huo, Coastal sasa inakuwa imejikusanyia jumla ya pointi 30 katika michezo 21 ikiwa imejichimbia katika nafasi ya nne mbele ya Prisons yenye pointi 28 katika michezo 21.
Soka Yanga yachanja mbuga ligi kuu
Yanga yachanja mbuga ligi kuu
Read also
