Na Hassan Kingu
Mechi iliyopigwa jana kati ya Yanga dhidi ya Azam imeendelea kuwa gumzo kwenye vijiwe mbalimbali, daladala, maofisini na kwingineko kutokana na mbungi kali isiyotarajiwa iliyopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kwa harakaharaka hakuna aliyetarajia kama mechi hiyo ingekuwa na msisimko wa aina ile na ingebaki kwenye kumbukumbu za wengi hata baada ya kumalizika kwa dakika 90.
Matokeo ya kupoteza mechi mbili za Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Yanga msimu uliopita yaliakisi Azam ni mnyonge mbele ya vijana wa Kariakoo kabla ya mwisho wa siku kuonyesha umwamba wake na matokeo kuisha kwa sare ya mabao 2-2 tena ikionekana lolote lingeweza kutokea zaidi kimatokeo.
Nachelea kusema mechi tuliyoishuhudia jana ilikuwa na kiwango cha hadhi ya kimataifa ya michuano mikubwa zaidi ya ligi ya ndani lakini tukaushuhudia mtanange huo ndani ya Ligi Kuu ya NBC, inasisimua mno.
Kwa aina ya wachezaji waliokuwa kwenye vikosi vyote viwili, ushindani waliokuwa wakiutoa, tambo zao tangu wanasajiliwa na hata ufundi waliokuwa wakiuonyesha ulikuwa ni wa hali ya juu na ilivutia kuwatazama.
Mara nyingi tumezoea kuona mechi za Azam na Yanga au nyinginezo zikiwa na wachezaji wengi wa kimataifa lakini huioni hiyo hadhi ya kimataifa kwenye mechi husika lakini kwenye mechi hiyo angalau imeonekana tena kwa kiwango kikubwa.
Lakini kabla ya yote kwanza niwape heshima wale mabeki wawili wa kati wa Azam; Malickou Ndoye na Daniel Amoah. Kama siyo ufundi wa Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Yanga kuamua kupiga mashuti nje ya 18 yaliyoipatia mabao Yanga basi mabao ya Ndoye na Amoah yangetosha kuamua mchezo.
Mabeki hao walifanya kazi mbili siku hiyo, kwanza walizuia kuhakikisha hakuna bao linalopatikana kwa washambuliaji wa Yanga kupenya kwao na kisha wakafunga mabao muhimu, hakika wanastahili pongezi. Amoah tunaufahamu uwezo wake lakini huyu Ndoye, Azam wamepata mtu.
Ahmada mwisho wa matatizo
Kupitia mechi ile na nyingine mbili za Azam zilizopita, unaweza kuungana na kauli hii kwamba Azam imepata mtu sahihi kwenye lango lao baada ya kuhangaika kwa misimu kadhaa kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Aishi Manula aliyetimkia Simba.
Ahmada ambaye ni raia wa Comoro kwanza analindwa na umbo lake na yeye pia analitendea haki, ‘anatisha’ golini na ana uhakika na mipira mingi anayoifuata.
Mabao yaliyofungwa na Fei yote alipambana kuufuata mpira ila kuna muda inapaswa kumpongeza mpigaji au mfungaji lakini kuhusu jitihada za Ahmada, alizionyesha na hakuwa na baya kwenye mechi ile, Azam imepata mkombozi wao golini.
Dube sio ‘Prince’ tena Azam
Prince Dube licha ya kuwa ni jina lake halali lakini ni kweli kwa msimu uliopita msaada aliokuwa akiutoa alikuwa ni kama Mwanamfalme ndani ya Chamazi. Mabao mengi yalipatikana kwake, usumbufu mwingi kwa wapinzani waliupata kwake.
Angalau kulikuwa na Rodgers Kola lakini hakufikia tishio la Dube kwa wapinzani na sasa kuna Tape Edinho ingawa alifunikwa na uwezo ulioonyeshwa na Kipre Junior, kuna Ayoub Lyanga pia ambaye ameimarika mno kwa sasa.
Hawa wote wanaweza kukuadhibu wakati wowote kutokana na aina ya uchezaji na ufundi walionao, usisahau nje kuna Tepsie Evance ambaye yeye hakucheza mechi hiyo, ni wazi Azam imebadilika mno na nahisi inakwenda kutupa ushindani ambao tulikuwa tukiuhitaji kutoka kwao miaka mingi iliyopita.
Sihitaji kumzungumzia sana Isah Ndala, mwanaume aliyekuwa na mamlaka ya juu kwenye kiungo cha kati akisaidiana na Sospeter Bajana. Ndala anaweza ‘kuendesha’, kukaba, kupiga pasi na kutumia nguvu pia, ni kiungo wa kisasa.
Fei Toto ni mmoja tu
Kabla ya kufika mbali, kwanza ni sahihi kumwita Feisal ‘Zanzibar Finest’, ni finest hasa. Anachokifanya sasa na umri alionao ni wazi tutayaona mengi kutoka kwake kuliko tuliyoyashuhudia kutoka kwa kaka zake ambao angalau nao walicheza kwa kiwango kikubwa kama Abdi Kassim Babi, Selemani Selembe, Abdulhalim Humud na wengine.
Fei alianzia benchi kwenye ule mchezo na aliingia kipindi cha pili, haikumchukua muda kupiga shuti lililojaa wavuni licha ya Ahmada kujaribu kuufuata mpira, dakika 20 baadaye anaandika bao la pili kwa mtindo huohuo na ndiyo aina ya mabao yake.
Yaani kile kilichoshindwa kufanywa na Stephane Aziz Ki, Fiston Mayele, Bernard Morrison kwa kupiga mashuti kadhaa nje ya 18 baada ya kushindwa kuipenya ngome ya Azam, kilikuja kufanywa na Zanzibar Finest kwenye ubora wa hali ya juu.
Fei aliingia na kuamua matokeo, akaubeba mchezo mgongoni mwake na kuhakikisha Yanga haivunji rekodi yake ya kutofungwa tangu kuanza kwa msimu uliopita ingawa walikosa ‘clean sheet’.
Uprofesa wa Nabi
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi aliyepewa cheo cha uprofesa na mashabiki wa Yanga kutokana na kuridhishwa na kazi yake, alijitahidi kudhihirisha kuwa jina hilo hakupewa bure na alipambana kulitendea haki katika mechi ile.
Kumuanzisha Fei nje haikumaanisha hakuwa na kiwango cha kucheza mechi ile iliyokuwa imejaa wachezaji wa mataifa ya kigeni, isipokuwa alifahamu alihitaji ‘mbegu’ nje ya kwenda kumaliza mzizi wa fitna mambo yanapokuwa magumu.
Iko wazi kuwa Yanga ilivyo ni lazima imzunguke Fei kupitia Mayele kwa maana ya kupika mabao na kuipa pointi muhimu timu, hivyo kumuweka nje kulimpa muda Fei kuiona mechi ile na mwisho kupewa majukumu ya nini cha kufanya ili mambo yasiharibike.
Kipindi cha pili Nabi alimtoa Denis Nkane na kumuingiza Fei kisha akamtoa Dick Job aliyeanza beki wa kulia na kumuingiza Djuma Shaban. Maana yake ni kwamba spidi ya Yanga ilikuwa inakwenda kubadilika na mashambulizi yangeongezeka maradufu na ndicho kilichotokea.
Hata ‘sub’ ya Gael Bigirimana na kumuingiza Salum Abubakar ‘Sureboy’ lilikuwa ni suala la kuongeza spidi na pasi nyingi kwa wapinzani. Kwa kifupi alichanga karata zake vyema kuhakikisha anaendana na presha ya vijana wa Azam ambao nao kila mmoja alijitutumua kumuonyesha kocha mpya wa timu hiyo aliyekuwa jukwaani, Mfaransa Denis Lavagne.
Arajiga gumzo kila kona
Mwisho kabisa kukaibuka gumzo la mwamuzi wa mchezo, Ahmed Arajiga kila mmoja akiongea lake kuhusiana na maamuzi ya baadhi ya matukio ya mechi hiyo.
Kama vile rafu za Bajana ambaye anaonekana alistahili kadi nyekundu au njano mbili au penalti inayodaiwa ya Dube dhidi ya Mwamnyeto, kuna ile penalti aliyokosa Djuma baada ya Morrison kudondoshwa eneo la hatari na ile ya mpira wa Joyce Lomalisa anaodaiwa kupiga krosi ukiwa umeshatoka nje.
Binafsi bila ya kujali kamati za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litaeleza nini juu ya Arajiga, lakini sioni tatizo lake popote, namuona kama ni mwamuzi wa daraja la juu Tanzania aliyecheza mechi ngumu ambayo kama angepewa mwamuzi mwingine sidhani kama tungefaidi kuona lile ‘bonge la mechi’ linalosifiwa mpaka leo.
Aina ya wachezaji aliokuwa akiwaamua na aina ya soka walilokuwa wakicheza lililojaa ubabe, ujanja na akili nyingi inapaswa kuwa somo juu ya ukuaji wa soka tulilonalo na aina ya waamuzi tunaopaswa kwenda nao au kuwazalisha kwa ajili ya miaka ijayo.
Kiwango cha mechi tuliyoishuhudia, misimu ya baadaye kidogo kama tutakuwa makini inaweza kuwa ndiyo ‘levo’ ya takriban mechi zote za Ligi Kuu, hivyo tusiishie kumlaumu mwamuzi tuangalie nini kifanyike ili twende sawa na spidi na kasi ya soka tunalolitaka kwetu.
Kama binadamu mwingine, Arajiga hawezi kuwa hajakosea hata kidogo hasa ukizingatia ubora wa mechi aliyokuwa akiichezesha lakini ni heri ya kikubwa alichokifanya kuliko makosa anayopewa ndani ya dakika 90 za mchezo ule utakaobaki kwenye kumbukumbu muhimu za msimu huu.
Wapo waamuzi wanatibua na kuvuruga mchezo mzima lakini ajabu mchezo huo unasifiwa na kuonekana ulichezeshwa kiume ingawa Arajiga anabebeshwa zigo la lawama ambazo bado inahitajika kutumia nguvu kubwa kumbebesha mgongoni mwake!
Kimataifa Achana na Arajiga, Yanga, Azam bonge la mechi
Achana na Arajiga, Yanga, Azam bonge la mechi
Read also