Na mwandishi wetu
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Ally Mayay amesema Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam utafungwa rasmi Mei, mwaka huu kwa takriban miezi miwili ili kufanyiwa matengenezo makubwa.
Licha ya uwanja huo kuelezwa ulishaanza matengenezo madogomadogo huku ukiendelea kutumika kwa mechi kubwa lakini Mayay amesema leo Jumanne kuwa uwanja huo utafungwa baada ya kuanza kwa matengenezo ya eneo la kuchezea.
Alisema matengenezo hayo ya ‘pitch’ ambayo yatasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kutokana na uwepo wa michuano ya Super Cup na ukarabati wake unatarajia kuwa wa wiki sita mpaka nane.
“Kuanzia mwezi wa tano hakutakuwa kabisa na matumizi ya Uwanja wa Mkapa sababu kutafanyika matengenezo makubwa, Caf watasimamia eneo la pitch na haya maeneo mengine atakuwepo mkandarasi kwa ajili ya ukarabati mkubwa pia wa maeneo mengine.
“Sababu kilichokuwa kinafanyika sasa hivi ni matengenezo ya baadhi kama vyumba vya kubadili nguo, media, vyumba vya waamuzi ambayo ni maboresho madogo lakini yale makubwa yataanza mwezi wa tano ambapo matumizi ya uwanja hayatokuwepo na inatarajia kuwa si chini ya wiki sita mpaka nane,” alisema Mayay.
Alisema hayo ni marekebisho ya kawaida kama ilivyoelezwa hapo awali kwani kiwango na ubora wa uwanja hutengenezwa na kutumika kulingana na nyakati husika lakini muda unavyozidi kwenda, inapaswa kufanyiwa maboresho kuendana na nyakati.
Kwa maelezo hayo, uwanja huo unaotumika kama uwanja wa nyumbani wa timu za Simba na Yanga, unatarajiwa kutumika na timu hizo kwenye mechi moja ya robo fainali za klabu Afrika kwa ile itakayopigwa hivi karibuni tu.