Na mwandishi wetu
Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama umetoa shukrani kwa uongozi na wanachama wa klabu ya Simba kwa kuchangia damu.
Wakati wa wiki ya Tamasha la Simba Day, mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kutoka mikoa mbalimbali walichangia jumla ya chupa 3,107 za damu, sawa na asilimia 155 ya lengo la kukusanya chupa 2,000 za damu katika mpango wa taifa wa damu salama.
Idadi ya chupa za damu zilizokusanywa kuanzia Julai 29 hadi Agosti ambapo mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa kinara kwa kukusanya chupa 532, Kigoma chupa 354, Mwanza 340, Tanga 263, Kagera 173, Dodoma 169, Mara 160, Pwani 152 na Geita 141.
Mikoa mingine ni Kilimanjaro ilikusanya chupa 114, Simiyu 108, Singida 105, Mbeya 90, Iringa 87, Njombe 85, Tabora 80, Rukwa 54, Songwe 36, Mtwara 24, Arusha 20 pamoja na Lindi 20.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally (pchani juu) leo Jumanne alisema kuwa lengo la Simba ni kuigusa jamii moja kwa moja pamoja na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii kama ilivyo dhima yao kila mwaka wanapoelekea kilele cha Simba Day.
“Kila mwaka tumekuwa tukifanya matukio haya ya kuchangia damu pamoja na kwenda kwenye jamii ya watu waliosahaulika, mwaka jana tulikuwa kwenye kituo cha wazee Nunge kule Kigamboni na mwaka huu tulikuwa kwenye shule ya watoto wenye ulemavu wa akili Sinza.
“Lengo letu ni kuwashika mkono wengine na hatutaishia hapa, tutaendelea kufanya hivi kila tutakapopata nafasi, tutaendelea kuwashika mkono wale wote wanaohitaji msaada,” alisema Ally.
