Na mwandishi wetu
Baada ya hitilafu ya umeme kutokea kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam jana kwenye mchezo wa Taifa Stars na Uganda, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay amesema suala hilo litatolewa taarifa rasmi.
Mayay hata hivyo hakufafanua zaidi kilichotokea zaidi ya kukiri kuwa umeme ulikatika maeneo ya Temeke lakini alisisitiza kuwa taarifa ya wataalam kuhusiana na hitilifau hiyo itatolewa.
Katika mchezo huo wa kuwania kufuzu kushiriki fainali za Mataifa Afrika (Afcon) 2023 na kuisha kwa Stars kufungwa bao 1-0, mechi hiyo ililazimika kusimama kwa zaidi ya dakika 30 kabla ya baadae kuendelea.
“Sio taa za uwanja kutokuwa na nguvu, hapana isipokuwa umeme ulikuwa umekatwa kwa hiyo ishu hiyo tutatoa taarifa rasmi ya kueleza hali hiyo ambayo itakuwa ni taarifa ya kitaalam, wataalam wenye mamlaka hayo wanaojua vipengele vya masuala ya umeme watatoa taarifa,” alisema Mayay.
Mayay aliyewahi pia kuichezea Taifa Stars alitoa maoni kuhusu Stars kupoteza mchezo huo akiamini pamoja na matokeo hayo lakini bado Stars ina nafasi ya kufuzu.
“Ni kweli jana haikuwa siku nzuri sababu matarajio yalikuwa makubwa ukizingatia mechi ya kwanza tulipata alama tatu ugenini kwa hiyo matarajio yalikuwa kupata tena alama tatu nyumbani lakini ndio soka matokeo hayatabiriki siku zote,” alisema.
“Maana angalau tungepata sare japo bado nafasi ipo mpaka sasa ingawa ugumu umezidi kuongezeka kwenye mechi mbili zilizobaki lakini mimi naamini tumepata cha kujifunza, tumeumia lakini kwamatokeo kama haya unapaswa kuchukua kitu cha kujifunza siku za usoni,” alisema Mayay.
