Mshahara kumtoa Ronaldo Man United
London, England
Dhamira ya Cristiano Ronaldo kuondoka katika klabu ya Manchester United iko pale pale licha ya ugumu uliopo na sasa inadaiwa yuko tayari kupunguziwa mshahara kwa asilimia 30 ili tu aondoke katika klabu hiyo.
Wakala wa Ronaldo, Jorge Mendes amepania kumtafutia mchezaji huyo timu nyingine ya kujiunga nayo licha ya kocha mpya wa Man United, Erik ten Haag kusisitiza kwamba hawana mpango wa kumuuza.
Mendes pia tayari anafahamu kwamba klabu za Chelsea na Bayern Munich ambazo Ronaldo alionekana kuwa tayari kujiunga nazo zimeshafuta mpango wa kumchukua na hapo hapo Ronaldo mwenyewe anadaiwa kukataa ofa inayotajwa kuwa ni nono ya kucheza soka nchini Saudi Arabia.
Ronaldo pia amewahi kuhusishwa na ofa ya kujiunga na klabu ya Atletico Madrid ikidaiwa kwamba kocha Diego Simeone anashawishika kumchukua mchezaji huyo ili kuimarisha kikosi chake lakini hapo hapo habari nyingine zinadai kwamba usajili wa Ronaldo katika klabu hiyo unaonekana kama ni kujiingiza katika matatizo ya kifedha ambayo klabu hiyo haiwezi kuyamudu.
Habari za ndani pia zinadai kwamba Mendes aliwahi kumpigia chapuo mchezaji huyo ili ajiunge na Barcelona kabla timu hiyo haijamsajili Robert Lewandowski anayetokea Bayern Munich na hapana shaka klabu hiyo haitomhitaji tena Ronaldo baada ya kumpata Lewandowski.
Na sasa Mendes ameamua kuingia na gia ya kupunguza mshahara wa mchezaji huyo wa Ureno kwa asilimia 30 kama mbinu ya kuzishawishi klabu ambazo zinaweza kushawishika kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 ili tu aondoke Old Trafford.
Ronaldo pamoja na umri kuwa mkubwa lakini anaonekana bado ana makali kwani katika msimu wa 2021/22 aliifungia Man United jumla ya mabao 24 katika mashindano mbalimbali na ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo na hapana shaka, Ten Haag anaamini mchezaji huyo anaweza kuwa msaada kwake katika msimu wa 2022/23 utakaoanza baadaye mwezi ujao na ndio maana hataki kuona akiondoka.
Sifa hizo ndizo ambazo Mendes anaamini zinaweza kumrahishia kumpigia chapuo mchezaji huyo kujiunga na klabu nyingine hasa zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwa Ronaldo anataka kushindana katika mashindano hayo hapo hapo akiziangalia fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazofanyika Qatar kuanzia Novemba mwaka huu.
