Manchester, England
Klabu ya Manchester United kwa sasa ipo njia panda kuhusu mambo ya baadaye ya kipa wao, Andre Onana ambaye mshahara wake unatarajia kupaa baada ya Septemba mwaka jana kumtoa kwa mkopo katika klabu ya Trabzonspor ya Uturuki.
Ongezeko la mshahara wa kipa huyo wa kimataifa wa Cameroon litachangiwa na timu hiyo kufuzu kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kwa mujibu wa makubaliano, kipa huyo anatarajia kurudi Man United baada ya msimu huu.
Mpango wa kipa huyo kwenda Trabzonspor kwa msimu huu ulifanikishwa kama sehemu ya mkakati wa kumpunguzia mshahara baada ya Man United kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2025-26 na hakukuwa na makubaliano ya kumfanya apate usajili wa kudumu kwenye timu hiyo ya Uturuki.
Kwa mantiki hiyo, Onana anatarajia kurudi Man United na kwa kuwa timu hiyo ipo nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu England, upo uwezekano mkubwa wa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na mshahara wa Onana unatarajia kurudi katika kiwango chake cha zamani.
Mazingira yaliyopo yanasababisha uwezekano wa kummalizia Onana mshahara wake kama kutakuwa na mpango mwingine wa kujadili mkataba mwingine ingawa hapo hapo Man United ipo katika mkakati wa kupunguza gharama za mishahara.
Onana, 29, nyota wa zamani wa Inter Milan, alisajiliwa Man United mwaka 2023 wakati wa kocha Erik ten Hag na amebakisha miaka miwili katika mkataba wake wa sasa na Man United.
Shauku kubwa ya Onana ni kurudi Man United kupigania namba ingawa kipa namba moja wa sasa, Senne Lammens anaonekana kumvutia kocha Michael Carrick ambaye hana mpango wa kusajili kipa mwingine badala yake anapiga hesabu za kumpata mbadala wa kipa namba mbili wa timu hiyo, Altay Bayindir.
Kimataifa Mshahara wa Onana pasua kichwa
Mshahara wa Onana pasua kichwa
Read also
