Na mwandishi wetu
Mabingwa wa Ligi Kuu NBC, Yanga SC wataanza mchezo wa kwanza wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, Agosti 9 na mchezo wa pili utakuwa baina ya Simba na Singida Fountain Gate, Agosti 10, mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa leo Jumamosi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeonesha michezo hiyo yote mpaka ule wa fainali wa Agosti 13, mwaka huu yote itapigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Ngao ya Jamii ambayo huashiria kuanza kwa msimu mpya wa ligi, safari hii itapigwa kwa mtindo huo wa timu nne wakati awali ilihushisha timu mbili ambazo ni bingwa wa Ligi Kuu NBC dhidi ya bingwa wa Kombe la FA (ASFC).
Singida F.G inakutana na Simba ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mara moja na sare moja katika michezo ya ligi msimu uliopita wakati Azam wao wana kumbukumbu mbaya ya kufungwa kwenye fainali ya FA iliyochezwa Tanga mwezi uliopita na kwenye michezo ya ligi msimu uliopita walifungwa na Yanga mchezo mmoja na sare moja.
Ngao ya Jamii mara kadhaa huwa ni fursa ya mashabiki pia kushuhudia timu hizo zikiwa na nyota wapya waliosajiliwa na wengine waliohama kutoka timu moja kwenda nyingine.
Mbali na wachezaji wapya kwa Yanga watakuwa na kocha mpya, Muargentina, Miguel Gamondi wakati Azam itakuwa chini ya kocha mpya, Youssouph Dabo raia wa Senegal.
Soka Yanga kuanza na Azam FC Ngao ya Jamii
Yanga kuanza na Azam FC Ngao ya Jamii
Read also