Istanbul, Uturuki
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amekataa kumlaumu kipa wake, Andre Onana licha ya kufanya makosa mawili yaliyosababisha timu hiyo itoke sare ya mabao 3-3 na Galatasaray katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika mechi hiyo ya Kundi A, Man United ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 na baadaye kuongoza kwa 3-1 kabla Onana hajafanya makosa mawili yaliyofanya ubao usomeke 3-3.
Matokeo hayo yanazidi kuiweka Man United katika wakati mgumu kuweza kufuzu hatua ya mtoano kwani hadi sasa timu hiyo inaburuza mkia katika kundi lake huku Onana akilaumiwa kwa kukosa umakini wa kudhibiti mipira ya mbali iliyopigwa na Hakim Ziyech.
Ten Hag hata hivyo alipoulizwa na waandishi kuhusu Onana kwanza alijibu kwa kifupi, “Yuko sawa.” na baada ya hapo akasisitiza kwamba si kosa la mtu mmoja.
“Kama nilivyopata kusema si suala la mtu mmoja, ni kweli kwamba makosa ya mtu mmoja mmoja kwenye soka yanaweza kubadili mambo na mtu anabeba lawama lakini wakati wote ni suala la timu,” alisema Ten Hag.
Ten Hag alisema kwamba timu yake ni nzuri, wachezaji wote katika kikosi ni wazuri na wanahitaji kupewa heshima kwa kuichezea Manchester United, kwa sababu ni wachezaji mahiri na hilo linawahusu wachezaji wote.
Man United bado haijatoka katika mbio za kusaka tiketi ya hatua ya mtoano (16 bora) ya Ligi ya Mabingwa licha ya kushinda mechi moja tu kati ya tano, nafasi ya kusonga mbele ipo japo ndogo.
Matokeo mechi za jana Jumatano Ligi ya Mabingwa Ulaya…
Galatasaray 3-3 Man Utd
Sevilla 2-3 PSV Eindhoven
Bayern Munich 0-0 FC Copenhagen
Arsenal 6-0 Lens
Real Madrid 4-2 Napoli
Sporting Braga 1-1 Union Berlin
Benfica 3-3 Inter Milan
Real Sociedad 0-0 RB Salzburg
