Manchester, England
Nahodha wa Man United, Bruno Fernandes (pichani) amesema ataifikiria hatma yake katika kikosi cha timu hiyo baada ya fainali za Euro 2024 ambapo atakuwa akiiwakilisha timu ya taifa ya Ureno.
Fernandes amesisitiza kwamba kwa wakati huu akili yake inafikiria mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Man City itakayopigwa Mei 25 pamoja na kuipigania Ureno kwenye fainali za Euro 2024 nchini Ujerumani.
Kauli ya Fernandes, 29, imekuja baada ya kuwapo uvumi kwamba anaweza akaachana na klabu hiyo lakini alipoulizwa kuhusu majaliwa yake katika klabu hiyo alisema kwa sasa hafikirii suala hilo ambalo si lake yeye binafsi bali linahusisha watu wengine.
“Kwa hiyo kama mtataka niwe wazi, kama mnataka nifikirie kuhusu kuendelea kuwa kwenye Ligi Kuu England sitakuwa na la kusema kwa sasa hadi baada ya fainali za Euro,” alisema Fernandes.
Fernandes alisema kwamba Man United inaweza kumaliza msimu na kulibeba taji la FA na hapo watakuwamo kwenye michuano ya Ulaya jambo ambalo ni muhimu mno kwao.
“Kwa sasa hakuna kitakachonitoa kwenye mbio za ubingwa, kwenye mbio za Kombe la FA na fainali za Euro, hakuna kilicho muhimu zaidi ya hayo kwa wakati huu,” alisisitiza Fernandes.
Fernandes ambaye huu ni msimu wake wa tano ndani ya kikosi cha Man United alisema kwamba anajiona bado ni mchezaji anayehitajika katika kikosi hicho cha Old Trafford.
Machi mwaka huu mchezaji huyo alisema kwamba alikutana na wamiliki wapya wa klabu hiyo na kuwaambia kuwa angependa kuendelea kubaki na klabu hiyo ambayo ana mkataba nayo hadi Juni, 2026 na kwa msimu huu hadi sasa ana mabao 15 katika mechi 45.