Na mwandishi wetu
Rais wa Klabu ya Singida Fountain Gate, Japhet Makau (pichani) amewashukuru wachezaji wa timu hiyo kwa kuanza na ushindi wa kishindo wa mabao 4-1 dhidi ya JKU katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar.
Makau ameyasema hayo akieleza kuwa msimu huu wana dhumuni la kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita katika michuano hiyo, hivyo ushindi huo umeonesha wako sehemu salama katika mipango yao.
“Unajua safari hii tumekuja kwa umakini mkubwa zaidi ya mwaka jana ambapo tuliishia fainali, kwa hiyo tunataka kufanya vizuri zaidi na ili kufanya vizuri lazima uanze vizuri, ndio maana tunawashukuru vijana wameanza vizuri kwa ushindi mkubwa na hii inatupa furaha,” alisema Makau.
Alisema walifahamu mechi ya JKU itakuwa ngumu kutokana na kukutana awali kwenye mechi za awali za Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ambapo mechi ya kwanza Singida FG ilitoka na ushindi wa mabao 4-1 kabla ya JKU kushinda 2-0 mechi ya marudiano.
Makau alisema hata hivyo wanashukuru wamewafunga kwenye mechi ya jana Ijumaa iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Katika michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyopita, Singida FG ilifanikiwa kutinga hatua ya fainali lakini ilifungwa mabao 2-1 na Mlandege ya Zanzibar iliyobeba taji hilo.
Soka Rais Singida FG awashukuru wachezaji
Rais Singida FG awashukuru wachezaji
Read also