Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Simba, Suleiman Matola amesema siri ya ushindi wao dhidi ya Tabora United ilitokana na kuwasoma vyema wapinzani wao na kutumia udhaifu wao kufunga mabao.
Matola alisema hayo baada ya mchezo wao huo wa Ligi Kuu NBC uliochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora juzi na Simba kushinda mabao 4-0.
“Tuliwasoma Tabora United na kugundua wanapenda kwenda mbele na kuacha nafasi za pembeni wazi na sisi tukazitumia na kupiga krosi tukafanikiwa,” alisema Matola.
Naye kocha wa Tabora United, Goran Kopunovic alikubali kupoteza mchezo lakini akilia na nyasi za uwanja pamoja na makosa binafsi ya wachezaji wake.
“Ni kweli tumefungwa mabao 4-0 lakini nyasi zimechangia kwa sababu zilikuwa ndefu zikafanya mpira usitembee. Tabora na Simba zimetofautiana kwa ubora lakini kuwakosa wachezaji muhimu nako kumechangia kupoteza,” alisema Kopunovic.
Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 29 katika nafasi ya tatu ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja huku Tabora ikiendelea kusalia nafasi ya 12 kwa pointi 15.
