Manchester, England
Bilionea mpya aliyewekeza katika klabu ya Manchester United, Sir Jim Ratcliffe amesema inahitaji muda na subira kuirudisha klabu hiyo katika mafanikio yake ya zamani.
Ratcliffe ambaye ni bilionea wa nchini Uingereza na mzaliwa wa jiji la Manchester, alikubali kununua hisa asilimia 25 katika klabu hiyo kwa thamani ya Pauni 1.03 bilioni kupitia kampuni yake ya Ineos.
Kampuni ya Ineos ambayo itasimamia uendeshaji na usimamizi wa soka pia itawekeza Pauni 236 milioni kwa ajili ya maendeleo ya uwanja wa klabu hiyo wa Old Trafford.
Katika taarifa yake Ratcliffe aliwaambia mashabiki wa klabu hiyo kwamba wao Ineos wanajua wajibu wao kwa kuwa walezi wa klabu hiyo kwa niaba ya mashabiki.
“Naamini tunaweza kuleta maendeleo kwenye michezo ili kuendana na mafanikio ya kibiashara ambayo hakuna shaka kuwa klabu imekuwa ikiyafurahia,” alisema Ratcliffe na kuongeza, “Yote hayo yatahitaji muda, subira pamoja na usimamizi mzuri wa kitaalamu.”
“Mna shauku kubwa na Manchester United, na sisi hivyo hivyo, hakuna uhakika wa moja kwa moja katika michezo na mabadiliko yanahitaji muda, nasi tuko hapa kwa ajili ya hilo, pamoja tunataka kusaidia kuirudisha Manchester United mahali pake, katika kilele cha soka la England, Ulaya na dunia,” alisema Ratcliffe.