Barcelona, Hispania
Mshambuliaji nyota mpya wa Barca, Marc Guiu ambaye ndio kwanza ana miaka 17, amecheza mechi yake ya kwanza ya La Liga na timu hiyo na kufunga bao pekee na la ushinid dhidi ya Athletic Bilbao.
Giui (pichani juu) aliingia akitokea benchi katika dakika ya 79 kuchukua nafasi ya kinda mwenzake, Fermina Lopez na ilimchukua sekunde 33 kuipatia timu yake bao mara baada ya kuingia uwanjani.
Kwa bao hilo, Giui anakuwa amejiwekea rekodi ya kufunga bao la haraka na la kwanza katika historia ya timu hiyo kufungwa na mchezaji ambaye ndio kwanza anacheza mechi yake ya kwanza na timu hiyo.
Ushindi huo mwembamba wa jana Jumapili umeiweka Barca katika nafasi nzuri ya kuwafukuzia vinara na mahasimu wao Real Madrid kwani kwa sasa tofauti baina yao ni pointi moja na Jumamosi ijayo wataumana nao.
“Nilimwambia kwamba atakuwa na nafasi moja nzuri, napenda kuona sura za madogo hawa, hawana woga,” alisema kocha wa Barca, Xavi.
Xavi alichukua uamuzi wa kumpandisha Giui kikosi cha kwanza kama sehemu ya mkakati wake wa kukabiliana na janga la wachezaji majeruhi linalomkabili wakiwamo Robert Lewandowski na Frenkie de Jong.
Giui alijiunga na akademi ya Barca maarufu La Masia mwaka 2013, La Masia ni kituo maarufu duniani ambapo pia alipitia nyota wa zamani wa timu hiyo, Lionel Messi ambaye kwa sasa anaichezea Inter Miami FC ya Marekani.
Mastaa wengine waliopitia La Masia na kutamba katika klabu hiyo ni kocha Xavi mwenyewe, Andres Iniesta, Carles Puyol, Gerard Pique, Jordi Alba, Sergio Busquets, Cesc Fabregas (baadaye alihamia Arsenal) na wengineo.