Na mwandishi wetu
Ratiba ya mechi za nusu fainali ya Kombe la FA (ASFC) imewekwa wazi leo Alhamisi ambapo mechi ya kwanza kati ya Azam na Simba itapigwa Mei 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Mechi ya pili ya michuano hiyo imeelezwa kuwa itachezwa Mei 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Liti, Singida baina ya mabingwa watetezi, Yanga dhidi ya Singida Big Stars.
Ratiba hiyo iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), pia imeeleza kuwa michezo hiyo yote miwili itapigwa kuanzia saa 9.30 alasiri.
Kwa ratiba hiyo, Yanga sasa itakutana na Singida ndani ya wiki moja baada ya kupangwa kukutana tena Mei 4, mwaka huu kwenye mchezo wa Ligi Kuu NBC huku mechi zote mbili zikipigwa Uwanja wa Liti.
Singida ilitinga hatua hiyo baada ya kuifumua Mbeya City kwa mabao 4-1 wakati Yanga ilikata tiketi hiyo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold.
Simba ambayo itavaana na Azam wiki moja baada ya kumaliza mechi za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad AC ya Morocco, yenyewe iliingia nusu fainali kwa kuitandika Ihefu mabao 5-1.
Azam ambao ni mabingwa wa michuano hiyo msimu wa 2018-19 wao walipenya nusu fainali baada ya kuibamiza Mtibwa Sugar mabao 2-0.
Soka Simba, Azam kuvaana Mei 6
Simba, Azam kuvaana Mei 6
Read also