Madrid, Hispania
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema itakuwa kosa kubwa kuichukulia mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid kama ya kulipa kisasi badala yake iwe ni kuthibitisha uwezo wao wa kumfunga bingwa mtetezi.
Pep Badala yake aliwataka wachezaji wake kuitumia mechi hiyo kama nafasi ya kuthibitisha kwamba wanaweza kumfunga bingwa mtetezi na hatimaye kubeba taji la michuano hiyo ya klabu ambayo ni mikubwa na yenye utajiri.
Man City, usiku wa leo Jumanne itakuwa ugenini dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Real Madrid kwenye dimba la Santiago Bernabeu katika mechi ya nusu fainali ya kwanza.
Katika mechi ya leo Man City itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutolewa na Real Madrid katika hatua hiyo msimu uliopita ambapo baadaye Real Madrid ilikutana na Liverpool katika fainali na kuibuka kidedea.
“Hatuko hapa kwa ajili ya kulipa kisasi, tuko hapa kwa ajili ya fursa, kilichotokea siku za nyuma kimeshatokea, itakuwa kosa kubwa kuanza kulifikiria hilo kwa sasa,” alisema Pep.
“Somo tulilolipata mwaka jana si kwa ajili ya kulipa kisasi, ni kujifunza kuhusu kilichotokea, kupata matokeo mazuri, kucheza vizuri na kuiacha fursa kuufanya mchezo uwe wazi,” alisema Pep.
Msimu uliopita, katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya michuano hiyo, Man City ilianza na ushindi wa nyumbani wa mabao 4-3 na katika mechi ya marudiano ugenini ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Riyad Mahrez katika dakika ya 73.
Baadaye mambo yaliwaharibikia City kwa mabao mawili ya mshambuliaji wa Real Madrid, Rodrygo aliyetokea benchi na timu hizo kujikuta zikipambana katika dakika za nyongeza na Karim Benzema akazitumia vizuri kuipatia Madrid bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 95.
“Mimi si mtu wa kushabikia kuzungumzia mambo ya uzoefu kwa namna nzuri au mbaya, ni kweli tuna kocha yule yule na wachezaji asilimia 80 ni wale wale kwa timu zote lakini hizi ni mechi tofauti kabisa, tulicheza vizuri mechi ya nyumbani, tukiwa Madrid hatukucheza katika namna ya kipekee bali tulicheza vizuri, tulifanya kila tuliloweza ili kufika fainali lakini kilichotokea hayo ni mambo ya soka,” alisema Pep.
Nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya leo, Jumanne, Mei 09…
Real Madrid v Man City
Nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho, Jumatano, Mei 10…
AC Milan v Inter Milan