New York, Marekani
Wiki mbili baada ya maadhimisho ya miaka 27 ya kifo cha aliyekuwa rapa wa Marekani, Tupac Shakur ‘2Pac’, idara ya polisi nchini humo ilimkamata mtuhumiwa namba moja wa mauaji hayo, Duane ‘Keffe D’ Davis.
Keffe, 60 amekamatwa na kuelezwa kuwa miongoni mwa waliopanga njama za kumuua 2Pac aliyepigwa risasi usiku wa Septemba 7 kabla ya kufariki Septemba 13, 1996 baada ya damu kuvuja ndani kwa ndani kutokana na majeraha ya risasi hizo.
Hata hivyo, wakati kesi hiyo sasa inaibuka upya, kifo cha 2Pac kimeendelea kuhusishwa na mambo mengi ikiwemo ‘bifu’ mbalimbali alizokuwa nazo enzi za uhai wake.
Mfano, Keffe amekamatwa akiunganishwa kwenye kisanga kilichomhusisha mpwa wake, Orlando ‘Baby Lane’ Anderson ambaye kamera za ukumbi wa MGM Grand, Las Vegas zilimnasa akizozana na kina 2Pac muda mchache kabla ya kifo cha rapa huyo.
2Pac aliyekuwa akifanya kazi zake California, alikwenda Las Vegas, Nevada kwenye sherehe ya mshirika wake kibiashara, Tracy Robinson sanjari na kuhudhuria pambano la swahiba wake, Mike Tyson dhidi ya Bruce Seldon.
Lakini ghafla washirika wa bosi wa 2Pac, Suge Knight walipomwona Baby Lane eneo hilo walimwambia 2Pac kuwa jamaa huyo alijaribu kuwapora mwanzoni mwa mwaka huo na ndipo mzozo ulipoanza baina yao.
Baadaye 2Pac alirudi hotelini kwake, akajiandaa na kuondoka na Suge kuelekea kwenye klabu ya usiku, lakini wakiwa wamesimama katika barabara ya East Flamingo, ikaja gari aina ya Cadillac na kusimama upande aliokuwa amekaa 2Pac na kisha kumfyatulia risasi.
Risasi nne, moja mkononi, moja kwenye paja na mbili za kifua zilimpiga 2Pac, ambaye aliwahishwa hospitali na baada ya siku sita, alitangazwa kuaga dunia akiwa na miaka 25.
Polisi inadai kuwa Keffe, alikuwemo katika Cadillac hiyo iliyotekeleza mauaji hayo yaliyoihuzunisha tasnia nzima ya muziki duniani.
P. Diddy, The Notorious B.I.G
Licha ya Baby Lane ambaye naye aliuawa mwaka 1998 akiwa na miaka 23 kutajwa mno kwenye kifo hicho, lakini chuki baina ya West Coast ya Suge na East Coast chini ya Sean Combs ‘Diddy’ ilitajwa kuwa chanzo cha mauaji ya 2Pac.
Diddy aliyekuwa akimsimamia Christopher Wallace ‘B.I.G’ kupitia Lebo ya Bad Boys walitajwa kutokana pia na ugomvi wao wa awali.
B.I.G au Biggie Smalls alikuwa rafiki wa 2Pac kabla ya baadaye kuhitilafiana. Mwaka 1995, 2Pac aliliambia Jarida la Vibe kuwa Biggie alihusika aliposhambuliwa na kupigwa risasi Novemba 1994 alipokuwa mapokezi ya studio kwa ajili ya kwenda kurekodi.
2Pac alikwenda Quad Studio (Biggie na Diddy walikuwepo ndani) kurekodi ubeti kwa maelewano ya ujira wa Dola za Marekani 7,000 na mtayarishaji James Rosemond.
Akiwa mapokezi, alivamiwa na watu asiowajua ambao walimwibia na kumtishia, alipojaribu kupambana nao aliishia kupigwa risasi takriban tano lakini aliwahishwa hospitali na baadae kupona kabisa.
Tukio hilo liliongeza chuki baina yao ambapo baada ta Biggie kusikia amehusishwa na tukio hilo, aliamua kurekodi wimbo ulioitwa Who Shot Ya?
2Pac alikasirika mno, akitasfiri wimbo huo ni kama umemdhihaki na ndipo alipotengeneza wimbo wa Hit ‘Em Up unaotajwa kuwa wimbo bora zaidi wa Hip Hop wa ‘ku-diss’, ambapo aliwataja kwa majina maadui zake akilijumuisha pia Kundi la Junior M.A.F.I.A lililokuwa likiundwa na Lil Kim na Lil Cease wakati huo.
Mpaka leo, baadhi ya wadau wanaamini kifo cha 2Pac kilitokana na bifu hilo kabla ya kugongelewa muhuri kutokana na kifo cha Biggie akiwa California kwenye gari barabarani, gari aina ya Chevrolet ilimsogelea na kumfyatulia risasi.
Licha ya juhudi za madaktari usiku wa Machi 8 kuhangaikia uhai wake lakini Machi 9, 1997 ikatangazwa kuwa Biggie ameiaga dunia akiwa na miaka 24!
Mamlaka za juu Marekani
Ingawa hakujawahi kuwa na uthibitisho wa moja kwa moja lakini wanazi wa muziki wa 2Pac kutoka Marekani wamekuwa wakizitaja mamlaka za juu za nchi hiyo kama sehemu ya kumpoteza 2Pac.
Iko hivi, mpaka leo 2Pac au Makaveli anakumbukwa kwa uanaharakati wake dhidi ya uonevu wa mamlaka kwa jamii na mambo mengi yanayokinzana na maendeleo ya binadamu wa hali ya chini.
Nyimbo zake nyingi zililenga kufundisha, kuonya na kukanya juu ya hayo. Hata alipotoa albamu yake ya kwanza ya 2Pacalypse Now, aliyekuwa Makamu wa Rais Marekani wakati huo, Dan Quayle alisema hakukuwa na sababu ya kuachiwa kwa albamu kama hiyo akidai haina nafasi katika jamii.
Lakini 2Pac hakuwahi kusikia wala kuelewa juu ya makatazo hayo na ni kwa sababu alizaliwa chini ya wanaharakati, wakati huo marehemu mama yake, Afeni Shakur alikuwa na cheo kikubwa katika Chama cha Black Panther kilichokuwa kikipigania haki za mtu mweusi.
Pia alikuzwa vyema kiunaharakati na ‘Godfather’ wake, Geronimo Pratt ambaye alifariki akiwa Arusha, Tanzania mwaka 2011.
2Pac aliwahi kuingia kwenye mgogoro wa kupigana risasi na polisi akiwa Atlanta mwaka 1993, tukio lililohusishwa na ukosoaji wake mkubwa dhidi ya serikali.
Ilielezwa kuwa, 2Pac alikorofishana na polisi wawili ndugu; Mark na Scott Whitwell walipokuwa na wake zao siku ya mapumziko wakivuka barabara.
Ingawa kila upande ulijitetea kivyake lakini mashahidi wa tukio hilo waliiambia idara ya polisi kuwa kina Whitwell ndio walioanza kuwachokoza kina 2Pac na kuwafanyia vitendo vya kibaguzi.
Na walipoanza kuzozana polisi hao ndio walioanza kurusha risasi kabla ya 2Pac kujibu mapigo na kuwajeruhi polisi hao. Japokuwa kesi hiyo ilimalizwa lakini Mark aliamua kuacha kazi miezi saba baada ya tukio hilo.
Albamu ya mwisho
The Don Killuminati: The 7 Day Theory ya Novemba, 1997 ndio ilikuwa albamu ya mwisho kutengenezwa na 2Pac akiwa hai na ndipo alipoamua pia kufanya maamuzi ya kujitambulisha rasmi kama Makaveli.
Makaveli ni jina lililotoholewa kutoka kwa mwanasiasa wa Italia, Niccolo Machiavelli ambapo 2Pac alivutiwa na falsafa za Machiavelli alipokuwa akisoma vitabu vyake wakati yupo jela.
Inaelezwa albamu hiyo iliyotungwa na kuandikwa kwa siku tatu tu kabla ya kurekodiwa ndani ya siku nne, ilikuwa na ukosoaji dhidi ya jamii za siri za dini na hilo pia linatajwa kuwa miongoni mwa chuki nyingine za kimya kimya dhidi ya 2Pac ingawa wakati inatoka rasmi 2Pac alikuwa ameshafariki.
Upande wa wanaoamini kuwa 2Pac yuko hai amejificha sehemu, wanaeleza kuwa 2Pac aliiga mtindo wa Machiavelli aliyewahi kubuni kifo chake wakati huo.
Hakuna Tupac aliyezidi miaka 45
Kama ulikuwa hufahamu, jina halisi la 2Pac ni Lesane Parish Crooks lakini alipofikisha mwaka mmoja wazazi wake rasmi wakamwita Tupac Amaru Shakur akirithi jina la Tupac Amaru II aliyekuwa mwanamapinduzi wa Peru dhidi ya watawala Uhispania.
Amaru II aliuawa mwaka 1781 akiwa na miaka 43 kama alivyouawa Mfalme wa Inca (sasa Peru), Tupac Amaru mwaka 1572 akiwa na miaka 24 tu!
Tangu kifo cha 2Pac au MC New York kama alivyokuwa akitambulika miaka ya 1989 akiwa msanii chipukizi, hajasikika Tupac Amaru mwingine maarufu mpaka sasa.
Hollywood Miaka 27 ya utata wa kifo cha 2Pac
Miaka 27 ya utata wa kifo cha 2Pac
Related posts
Read also