Manchester, England
Manchester City hatimaye imekamilisha usajili wa winga Jeremy Doku kutoka Rennes ya Ufaransa kwa ada ya Pauni 55.4 milioni.
Doku mwenye umri wa miaka 21 amesaini mkataba wa miaka mitano, anajiunga Man City akiwa na rekodi ya kufunga mabao 10 katika mechi 75 za Ligi 1 nchini Ufaransa katika misimu mitatu iliyopita.
Baada ya kukamilisha usajili huo, Doku ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Ubelgiji akiwa ameichezea timu hiyo mara 16 hadi sasa, amekabidhiwa jezi namba 11.
“Hii ni siku kubwa kwangu, ni kubwa kwangu mimi binafsi pamoja na soka langu, City ni timu kubwa duniani, kwa hiyo kujiunga na timu hii ni tukio la kipekee,” alisema Doku.
Man City hadi kumpata winga huyo ilikuwa ikichuana na Chelsea na West Ham ambazo zote zilikuwa zikimtaka winga huyo ambaye alikuwa amekabiza miaka miwili katika mkataba wake na Rennes.
Klabu ya Rennes ilimsajili Doku, Oktoba 2020 kutoka Anderlecht ya Ubelgiji kwa ada ya Pauni 22 milioni, muda mfupi baada ya kuonekana akiichezea timu yake ya taifa.
Akizungumzia uamuzi wake wa kujiunga na Man City, Doku alisema kwamba ulichangiwa na hamu yake ya kutaka kufanya kazi na kocha Pep Guardiola.
“Mimi bado mchezaji mdogo, nina mengi ya kujifunza ili kuwa bora zaidi, kufanya kazi na Pep na wasaidizi wake pamoja na kucheza na wachezaji wa hadhi ya juu duniani kutanifanya niwe mchezaji bora, naona kuna uhakika katika hilo,” alisema Doku.
Naye mkurugenzi wa soka wa Man City, Txiki Begiristain alisema kwamba anaamini chini ya usimamizi wa Guardiola na wasaidizi wake, Doku atakuja kuwa mchezaji ya hadhi ya juu duniani.
Doku ni mchezaji wa tatu kusajiliwa na kocha Pep Guardiola wa Man City katika kipindi hiki cha majira ya joto, tayari amewasajili kiungo Mateo Kovacic kutoka Chelsea kwa ada ya Pauni 25 milioni na beki Josko Gvardiol kutoka RB Liepzig ya Ujerumani kwa ada ya Pauni 77 milioni.