Madrid, Hispania
Klabu ya Real Madrid imemuongezea mkataba wa mwaka mmoja kiungo wake mkongwe na fundi Luka Modric (pichani) ambaye sasa atakuwa na timu hiyo hadi mwaka 2024.
Modric mwenye umri wa miaka 37, mkataba wake na timu hiyo ulitarajiwa kufika ukomo katika siku za karibuni na tayari kulikuwa na habari kwamba alikuwa mbioni kujiunga na timu moja ya Saudi Arabia.
Kiungo huyo mkongwe ambaye Desemba mwaka jana alitamba na timu ya Taifa ya Croatia kwenye fainali za Kombe la Dunia akiifikisha timu hiyo nusu fainali, ameichezea Real Madrid mara 488 na kubeba matatu matatu ya La Liga.
Modric ambaye alitua Real Madrid kwa mara ya kwanza mwaka 2012 akitokea Tottenham pia ana mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na timu hiyo lakini pia mwaka 2018 alitwaa tuzo ya Ballon d’Or baada ya kuiongoza vyema Croatia hadi hatua ya fainali ya Kombe la Dunia.
Baada ya uamuzi wa kuongeza mkataba kufikiwa, Modric alitumia mtandao wa Twitter kufurahia uamuzi huo akipataja Real Madrid kama nyumbani pazuri pale aliposema, ‘Home Sweet Home.
Kwa uamuzi huo, Modric anaungana na wachezaji wengine walioongeza mikataba na klabu hiyo kina Toni Kroos, Dani Ceballos na Nacho Fernandez.
Real Madrid pia hivi karibuni imekamilisha usajili wa kiungo wa kimataifa wa England Jude Bellingham kutoka klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani.
Kimataifa Modric aongeza mwaka Real Madrid
Modric aongeza mwaka Real Madrid
Read also