Paris, Ufaransa
Winga wa PSG, Ousmane Dembele ameshinda tuzo ya Ballon d’Or kwa mwaka 2025 na kuwa mchezaji wa kwanza wa PSG kubeba tuzo hiyo akiwabwaga Mohamed Salah wa Liverpool na Lamine Yamal wa Barcelona.
Dembele ambaye alitwaa tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika usiku wa Jumatatu hii Septemba 22, 2025 jijini Paris, pia anakuwa mchezaji wa kwanza wa Ufaransa kubeba tuzo hiyo baada ya Karim Benzema kufanya hivyo mwaka 2018.
Kwa ushindi huo Dembele pia anakuwa mshindi wa 34 akiwa ameibeba tuzo hiyo kutoka kwa Rodri wa Man City ambaye aliibuka kinara mwaka 2024.
Baada ya kuandamwa na janga la kuwa majeruhi na kuonkeana kama ameanza kupoteza kiwango, mambo yalianza kumnyookea Dembele katika msimu uliopita, alicheza mechi 49 za PSG katika mashindano yote na kufunga mabao 33 huku akitoa asisti 15.
Katika msimu huo Dembele pia alimaliza Ligi Kuu Ufaransa maarufu Ligi 1 akiwa mfungaji bora mwenye mabao 21 katika mechi 29 za ligi hiyo.
Kubwa zaidi kwa Dembele hayakuwa mabao aliyofunga bali ubora wakati katika kutengeneza mashambulizi na kuwa mbunifu katika kila mechi aliyozocheza.
Kwa upande wa mataji, mchango wa Dembele haukujificha kwani PSG ilifanikiwa kubeba taji la Ligi 1, taji la Ufaransa na Ligi ya Mabingwa Ulaya walilolibeba kibabe kwa kuinyuka Inter Milan ya Italia mabao 5-0 katika mechi ya fainali.
Katika mechi hiyo ya fainali Dembele alitoa asisti mbili zilizozaa mabao ya Khvicha Kvaratskhelia na Desire Doue na hivyo kuwa mchezaji wa kwanza baada ya Marcelo kutoa asisti mbili kwenye mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika kipindi chote cha kulisaka taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, mchango wa Dembele ulikuwa wazi kwa kutoa asisti sita na kufunga mabao manane lakini anakumbukwa zaidi kwa bao lake lililoizamisha Liverpool na kwa bao la ushindi dhidi ya Arsenal katika mechi ya nusu fainali.
Dembele pia anakumbukwa kwa kufunga mabao matatu katika mechi moja (hat trick) kwa mechi mbili mfululizo, alianza katika mechi dhidi ya VfB Stuttgart kwenye Ligi ya Mabingwa na siku chache baadaye dhidi ya Brest katika mechi ya Ligi 1.
Kimataifa Dembele abeba Ballon d’Or
Dembele abeba Ballon d’Or
Read also
