Manchester, England
Mchezaji wa Manchester City, Phil Foden amesaini mkataba mpya na klabu hiyo utakaofikia ukomo mwaka 2027 hivyo kuongeza miaka mitatu mingine kwenye mkataba wake wa awali uliotakiwa kufikia ukomo mwaka 2024.
Foden mwenye umri wa miaka 22 hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao 52 katika mechi 182 tangu acheze mechi yake ya kwanza akiwa na timu hiyo Novemba 2017 akiwa ni mmoja wa wachezaji waliokuzwa na kuibukia kwenye akademi ya klabu hiyo.
“Ni vigumu kuzungumzia ni kwa namna gani nina furaha kwa kusaini mkataba huu mpya, ni ndoto iliyotimia, nimekuwa shabiki wa City kwa maisha yangu yote, nimekuwa nikifanya mazoezi hapa kwa miaka mingi na pia nimekuwa kijana muokota mipira,” alisema.
“Naipenda hii klabu sana, kwa hiyo ninapojua kwamba nitaendelea kuwa sehemu ya klabu hii hadi mwaka 2027 naona ni jambo la kipekee,” alisema Foden.
Foden, mzaliwa wa Stockport, mbali na Man City pia ni mchezaji anayeibukia kwenye timu ya Taifa ya England akiwa hadi sasa ameichezea timu hiyo jumla ya mechi 18 na kuifungia mabao mawili wakati huo huo ameshinda mataji 11 na City yakiwamo manne ya Ligi Kuu England, manne ya EFL na la FA.
Katika misimu miwili iliyopita, Foden ameshinda tuzo ya msimu ya mchezaji kijana wa Ligi Kuu England na ile ya mchezaji bora wa mwaka kijana ya Chama cha Wachezaji Profesheno.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola alimpa nafasi ya kuichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 17 na Foden hakuacha kumpongeza kwa jambo hilo, “Nimeendelea kuwa bora katika miaka ya karibuni na mengi kati ya hayo yamechangiwa na Pep na wasaidizi wake ambao wameniongoza kwa kila hatua kwenye uwanja wa mazoezi.”
Kimataifa Phil Foden aongeza mkataba Man City
Phil Foden aongeza mkataba Man City
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
