Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ameeleza kuwa mabadiliko ya wachezaji kipindi cha pili na uvumilivu waliokuwa nao kwenye mechi yao dhidi ya Polisi Tanzania ndiyo chachu ya ushindi wao wa mabao 2-1.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, waliibuka na ushindi huo jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha katika mchezo ulioonekana mgumu baada ya kutanguliwa kwa bao 1-0 kabla ya baadaye kupindua matokeo dakika za lala salama.
Nabi alisema kuwa walifahamu mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali ya hewa ya Arusha, uchovu wa mechi yao iliyopita ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na pia kukosa umakini kwa washambuliaji wake kwenye dakika za awali za mchezo huo.
“Tulikuwa tunajua mechi itakuwa ngumu kutokana na sababu tofauti, tumecheza mechi Jumamosi (dhidi ya Simba) tumetumia nguvu nyingi, kisha unakuja Arusha kwenye hali ya hewa tofauti lakini tunaamini pia dakika za mwanzo tungeweza kumaliza mchezo kama tungetumia nafasi.
“Hiyo ilikuwa ikiwapa nguvu wapinzani lakini kikubwa tulivumilia mpaka mwisho na kama ulivyoona kipindi cha pili tuliongeza nguvu kwa kuingia Makambo (Herritier), Morrison (Bernard) wakatupa nguvu ya kuibakisha nyuma Polisi muda wote na kupata matokeo,” alisema Nabi.
Nabi ambaye msimu uliopita aliweka rekodi ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara bila kupoteza mchezo wowote, amewataka washambuliaji wake kuongeza umakini zaidi ili kujihakikishia mapema pointi katika kila mchezo ulio mbele yao.
Kwa upande wa kocha wa Polisi, Joselin Shariff alisema vijana wake walijitahidi kupambana na kucheza kwa ustadi mkubwa kwa ajili ya kutafuta matokeo lakini makosa madogo madogo ndiyo yaliyowagharimu na kupelekea ushindi kwa wapinzani wao wenye uzoefu mkubwa.
“Mchezo wa mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, vijana wamepambana kadri walivyoweza lakini makosa ndiyo yaliyotugharimu na wapinzani kutokana na uzoefu walionao wakatuadhibu na wao kupata ushindi na kama unavyojua mpira una matokeo matatu,” alisema Joselin.
Soka Nabi ataja siri ya ushindi Yanga
Nabi ataja siri ya ushindi Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
