Na mwandishi wetu
Beki wa Taifa Stars, Dickson Job amewaahidi raha zaidi Watanzania kuelekea mchezo wao wa marudiano dhidi ya Uganda kuwania kufuzu fainali za Mataifa Afrika (Afcon) 2023.
Beki huyo amezungumza hayo leo Jumamosi baada ya kundi la kwanza la wachezaji wa timu hiyo kuwasili majira ya saa 6.30 mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Job aliyetoa pasi ya bao pekee ya mechi yao ya awali na Uganda iliyopigwa Uwanja wa Mamlaka ya Suez Canal, Misri, amewasili na wachezaji wengine saba, wengine walitarajiwa kuwasili usiku wa kuamkia leo pamoja na Kocha Mkuu, Adel Amrouche.
Alisema ushindi huo wa bao 1-0 umewapa mwanga kuelekea mechi inayofuata, akidai sasa watapambana kutafuta pointi tatu nyingine kwenye mchezo utakaopigwa Jumanne ijayo, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
“Ushindi tulioupata ni kitu kizuri kwa upande wetu sababu inatuonesha njia njema huko tunakoelekea, kikubwa ni kupambana kupata matokeo katika mchezo unaokuja ili kujiwekea mazingira mazuri kuelekea Afcon,” alisema Job.
“Tunahitaji mashabiki wajitokeze kwa wingi watusapoti vijana wao, tutapambana na tutawapa furaha zaidi,” alisema Job aliyechaguliwa mchezaji bora wa mechi ya juzi dhidi ya Uganda.
AKizungumzia pasi ya bao aliyoitoa kwa mfungaji Simon Msuva, alisema anaamini anazidi kuwa imara kila wakati na ataendelea kufanya marekebisho ili kuendelea kufanya vizuri na kuonesha ukubwa wa kipaji chake.
Stars sasa inashikilia nafasi ya pili ikiwa na pointi nne, nyuma ya Algeria yenye pointi tisa wakati Niger ni ya tatu kwa pointi mbili, Uganda inaburuza mkia kwa pointi moja.
Ili kuongeza hamasa katika mechi yao ya marudiano na Uganda, Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kutoa Sh milioni 10 kwa kila bao katika mechi tatu zilizobaki za Kundi F kuanzia mechi yao ya marudiano na Uganda.
Ahadi hiyo ni tofauti na ile iliyowekwa awali na Rais Samia ya kwamba atawapa Sh milioni 500 kama Stars itafanikiwa kutinga kwenye michuano hiyo inayotarajia kupigwa Ivory Coast.
