Doha, Qatar
Wajerumani hawaamini kilichowakuta Qatar, ushindi wa mabao 4-2 walioupata kwa Costa Rica haujawasaidia, wameaga mapema fainali za Kombe la Dunia na kuiacha Japan iliyoichapa Hispania mabao 2-1 ikisonga mbele.
Katika mechi hizo zilizochezwa jana Alhamisi, Ujerumani ilineemeka kwa mabao ya Serge Gnabry, Kai Havertz aliyefunga mawili na Nicklas Fullkrug wakati Costa Rica mabao yao yalifungwa na Yeltsin Tejeda na Manuel Neuer kipa wa Ujerumani ambaye alijifunga.
Ujerumani, mabingwa hao mara nne wa dunia wameishia nafasi ya tatu katika Kundi E na kushindwa kuyasogelea matumaini ya awali ya Taifa hilo kubwa kiuchumi na lenye historia kubwa katika soka kufika mbali ikikwamishwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Ujerumani ambao mwaka 2014 walibeba taji la Dunia kwenye ardhi ya Brazil, baada ya mafanikio hayo wamekuwa kama wenye mikosi, mwaka 2018 waliaga kwenye hatua ya makundi na 2022 wamerudia majanga yale yale.
Sura za wachezaji walio wengi wa Ujerumani akiwamo kocha wao mkuu, Hansi Flick baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, zilionyesha huzuni, kukata tamaa na kutoamini kilichotokea.
Matarajio ya awali katika kundi hilo ni kwamba Ujerumani na Hispania zingefuzu kupitia kundi hilo, Japan na Costa Rica zingeaga mapema, lakini imekuwa tofauti, Japan si tu kwamba imesonga mbele bali imesonga ikiwa kinara wa kundi ikiwa na pointi sita ikifuatiwa na Hispania yenye pointi nne sawa na Ujerumani huku Costa Rica ikishika mkia.
Hesabu za Ujerumani zilikuwa zikitegemea pia na ushindi wa mechi ya Japan na Hispania, ilitakiwa Hispania ishinde ili Japan ibaki na pointi tatu na Ujerumani iwe na pointi nne na kusonga mbele na Hispania lakini mambo yamekuwa tofauti.

Matokeo hayo yanaweza kutoa ishara ya kwamba Ujerumani si tena timu tishio katika soka au ni timu iliyoanza kukumbana na anguko, hivyo ni wakati wa kurudi nyumbani na kujiuliza kulikoni, ukiachana na maanguko ya fainali mbili za Kombe la Dunia, 2018 na 2022, hata Euro 2020, timu hiyo haikufika popote, ilitolewa hatua ya mtoano.
Ni wazi hatua ya kwanza ambayo Ujerumani itafanya ni kuachana na kocha Flick kabla ya mabadiliko mengine ya timu na nini kifanyike kuirudisha hadhi yake hasa kwa kuwa itakuwa mwenyeji wa fainali za Euro 2024, anguko jingine, tena la nyumbani, haliwezi kukubalika.
Matokeo Kombe la Dunia, mechi za jana Alhamisi
Kundi E
Costa Rica 2-4 Ujerumani T
Japan 2-1 Hispania
Kundi F
Canada 1-2 Morocco
Croatia 0-0 Ubelgiji
