Na mwandishi wetu
Licha ya Simba kuvutwa shati kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu NBC jana, kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mgunda amesema bado hawajakata tamaa ya kuwania taji.
Simba ilipata sare hiyo katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi ambapo matokeo hayo yanazidi kuacha pengo kati yake dhidi ya kinara Yanga.
Baada ya matokeo hayo, Simba imeendelea kusalia nafasi ya pili kwa pointi 64 baada ya mechi 27 huku Yanga ikiwa kileleni kwa pointi 71 baada ya mechi 27.
Mgunda alisema pamoja na matokeo hayo lakini wanasubiri hadi filimbi ya mchezo wa mwisho ndipo wanaweza kukata tamaa ya taji hilo.
“Haiwi mwisho mpaka ifike mwisho, tutarudi kujirekebisha kuendelea na mapambano katika michezo iliyobaki kujua hatma yetu ya ubingwa,” alisema Mgunda.
Kuhusu baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kupumzishwa kama Clatous Chama, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein na wengine waliokuwa benchi kuanza kikosi cha kwanza, Mgunda alisema wote walisajiliwa kwa ajili ya kuitumikia klabu hivyo walistahili kucheza.
Simba iliwapumzisha baadhi ya nyota wake muhimu huenda wakisubiri nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA) Jumapili hii ambapo watacheza na Azam FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
“Wachezaji wote waliocheza ni Simba na wana haki ya kuitumikia klabu yao na kutimiza majukumu yao. Kutocheza Chama ni sehemu ya mpangilio wa kazi, wote ni wa kwetu, kila mmoja tumpe nafasi ya kutumikia klabu na kuwaamini,” alisema Mgunda kocha wa zamani wa Coastal Union ya Tanga.