Rio de Janeiro, Brazi;
Brazil bado ina matumaini ya kumshawishi kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti ili akabidhiwe jukumu la kuinoa timu ya taifa hilo inayoongoza kwa kubeba Kombe la Dunia mara tano.
Ancelotti alianza kuhusishwa na Brazil Desemba mwaka jana mara baada ya timu hiyo kukwama katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia ikitolewa kwa mikwaju ya penalti na Croatia.
Baada ya Brazil kutolewa kwenye michuano hiyo iliyofanyika Qatar, aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Tite aling’atuka na ndipo jina la Ancelotti lilipochomoza ikiaminika kuwa anafaa kupewa jukumu hilo.
Ancelotti hata hivyo alijiweka kando na mjadala huo ingawa nchini Brazil nako kukaibuka mjadala wa kama ni sahihi timu hiyo kunolewa na kocha ambaye si raia mzawa wa Brazil.
Katika mjadala huo wapo wanaodhani huu ni wakati sahihi kwa Brazil kuwa na kocha wa kigeni baada ya mambo kutokuwa mazuri ingawa pia wapo wanaoamini si sahihi kufanya hivyo kwani timu hiyo inahitaji Mbarazil anayelijua vizuri soka la nchi hiyo na mahitaji yake.
Ancelotti hata hivyo ameonekana kutoichangamkia kazi ya kuinoa Brazil na hivi karibuni baada ya Real Madrid kutolewa katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, alinukuliwa akisema kwamba amehakikishiwa kuwa ataendelea kuinoa klabu hiyo iliyotwaa taji hilo msimu uliopita.
Tangu kuondoka kwa Tite, Brazil bado haijachagua kocha wa kudumu huku kukiwa na habari kwamba mabosi wa shirikisho la soka nchini humo yaani CBF safari hii wanataka kumpa kazi kocha kutoka nje ya taifa hilo.
Kimataifa Brazil yamkomalia Ancelotti
Brazil yamkomalia Ancelotti
Read also