Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amemjia juu Jamie Carragher kwa maoni ambayo amekuwa akitoa kuhusu timu hiyo baada ya kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Fulham na kudai kuwa ni maoni yaliyojaa ubinafsi.
Carragher alihoji namna timu ya Man United ilivyopangwa na kucheza katika mechi hiyo na Ten Hag amekiri kwamba beki huyo wa zamani wa Liverpool alikuwa na hoja lakini amekuwa ni mtu wa kukosoa mwanzo mwisho.
“Kuna wachambuzi wana hoja katika maoni yao, wana ushauri mzuri lakini kuna wengine wana mambo yao binafsi, Jamie Carragher tangu mwanzo amekuwa bingwa wa kukosoa na sasa anachotaka ni kufikisha hoja yake,” alisema Ten Hag.
Carragher alisema kwamba Man United inakaba kwa namna ambayo hakuwahi kuiona, ilikuwa ikicheza kwa udhaifu nyuma na kushambulia kwa kasi hali iliyoacha eneo la kati kuwa wazi na Fulham kulitumia.
“Labda katika dakika 30 za kwanza, hapo anaweza kuwa na hoja, Fulham katika eneo la kiungo kidogo walishangaza lakini tulilazimika kutafuta suluhisho, baada ya hapo tulipata suluhisho,” alisema Ten Hag ambaye timu yake leo Jumatano itaumana na Nottingham katika Kombe la FA.
Ten Hag hata hivyo alikiri kutoridhishwa kwa namna ambavyo timu yake ilikuwa ikikaba katika mechi hiyo iliyopigwa jana Jumanne usiku hasa upande wa kushoto hasa katika dakika 30.
Alisema kwamba waliruhusu eneo lao kushambuliwa ingawa aliwatetea wachezaji wake akisema kwamba wanasoka si kama roboti, kuna wakati wanakuwa na siku mbaya.
Kimataifa Ten Hag amtolea uvivu Carragher
Ten Hag amtolea uvivu Carragher
Read also