Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya wasichana chini ya miaka 20, Tanzanite Queens, Bakari Shime amesema wanaenda kwenye mashindano ya Afrika wakiwa na nia moja ya kurudi nyumbani na kombe.
Mashindano ya Afrika yanatarajia kuanza Ijumaa hii mjini Accra, Ghana huku Tanzanite ikianza mashindano hayo kwa kuikabili timu ya taifa ya Uganda.
Akizungumza Dar es Salaam Jumatatu hii, Shime alisema kwamba wamejiandaa vizuri na wachezaji waliojumuishwa kwenye safari hiyo wako vizuri, kikubwa kwao ni kuangalia jinsi gani wataanza mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda.
“Ni matumaini yangu kuwa tuna nafasi ya kufanya vizuri kwa kuwa Uganda si wageni kwetu, ni majirani zetu tunafahamiana sana, tumecheza nao katika mashindano yaliyopita ya Cecafa na kupata ushindi.
“Lakini haya ni mashindano mengine kikubwa ni kuhakikisha wasichana wanakuwa na hali nzuri na morali ya kujituma na kupambana ili tufanye vizuri,” alisema Shime.
Alisema hawapaswi kucheza na historia zaidi ya kuangalia mashindano jinsi yalivyo na namna gani ya kucheza, cha msingi wao wana wachezaji wenye uzoefu ambao wamecheza kwa muda mrefu na ni matumaini yao watafanya vizuri.