Barcelona, Hispania
Kampuni ya DIS ya nchini Brazil inataka mshambuliaji wa PSG, Neymar afungwe jela miaka mitano katika kesi ya rushwa na ubadhirifu inayomkabili ikihusisha usajili wa mchezaji huyo kutoka klabu ya Santos ya Brazil kwenda Barcelona mwaka 2013.
DIS, kampuni inayojihusisha na masuala ya uwekezaji, kwa kipindi hicho ilikuwa ikimiliki asilimia 40 ya haki za mchezaji huyo, inadai kwamba ilipoteza haki hizo kwa sababu thamani halisi ya mchezaji huyo ilishushwa.
Neymar mwenye umri wa miaka 30 sasa alikana kufanya kosa lolote lakini mwaka 2017 alishindwa rufaa yake katika Mahakama Kuu nchini Hispania hali iliyowafanya waendesha mashtaka kulirudisha mahakamani shitaka hilo.
Kutokana na hali hiyo, taarifa za mahakama zilieleza kwamba Neymar sasa atalazimika kufika mahakamani Jumatatu mjini Barcelona kwa mara ya kwanza yeye mwenyewe ingawa haijaeleweka kama atatakiwa kufika mahakamani hapo kila siku kwa wakati wote kwa kipindi cha wiki mbili za usikilizwaji wa shitaka hilo.
Katika shitaka hilo mashahidi wengine wa mshitakiwa ni pamoja na wazazi wa Neymar, klabu za Santos na Barcelona, marais wa zamani wa klabu ya Barcelona, Josep Maria Bartomeu na Sandro Rosell pamoja na rais wa zamani wa klabu ya Santos, Odilio Rodrigues. Kati ya viongozi hao wote ni Rosell pekee aliyewahi kujitokeza hadharani akikana kufanya kosa lolote.
Kwa upande wake wakili anayeiwakilisha familia ya Neymar, Baker McKenzie alisema kuwa mahakama za Hispania hazina uhalali wa kuihoji familia ya Neymar na kampuni yao ya N&N kwa sababu makosa wanayohusishwa nayo watuhumiwa yalifanywa na raia wa Brazil nje ya mamlaka za Hispania. Pia alidai kwamba tuhuma za jinai wanazohusishwa nazo hazina adhabu nchini Brazil.
DIS walipata asilimia ya haki za Neymar wakati akiwa na miaka 17 kwa malipo ya Euro 2 milioni wakati Barcelona wanadai kwamba wakati mchezaji huyo akisajiliwa ada ya uhamisho ilikuwa Euro milioni 57.1 ambapo kati ya hizo Euro 40 milioni zililipwa kwenye familia ya mchezaji huyo. DIS walipata asilimia 40 ya mgao wa Euro 17 milioni zilizobakia ambazo ndizo zilizolipwa katika klabu ya Santos.
“Haki za Neymar hazijauzwa kwa mtu aliyetaka kulipa fedha nyingi, kuna klabu ambazo zilimtaka zikiwa tayari kutoa zaidi ya Euro milioni 60,” alisema wakili wa DIS, Paulo Nasser.
Mbali na kifungo cha miaka mitano jela, DIS pia wanataka adhabu ya kifungo kwa mabosi wa Barcelona, Rosell na Bartomeu pamoja na faini ya Euro 149 milioni.
Waendesha mashitaka nchini Hispania wanataka Neymar afungwe miaka miwili jela pamoja na faini ya Euro 10 milioni na kifungo cha miaka mitano jela kwa Rosell na faini ya Euro milioni 8.4 kwa klabu ya Barcelona.
Akifafanua zaidi wakili wa familia ya Neymar, Baker McKenzie alisema familia hiyo inashitakiwa kwa rushwa inayohusisha watu binafsi inayohusisha ushindani wa bidhaa na huduma kati ya makampuni wakati Neymar si bidhaa au mali, ni binadamu anayeongozwa na utashi wa kuchagua anachotaka na zaidi ya hilo wakili huyo alisema uhamisho wa mchezaji huyo haujavunja sheria yoyote ya Fifa.
Kimataifa Neymar atishiwa kufungwa miaka mitano jela
Neymar atishiwa kufungwa miaka mitano jela
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
