Barcelona, Hispania
Mahakama moja ya Hispania imeagiza beki wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Gerard Pique ahojiwe akihusishwa na tuhuma za rushwa iliyosababisha mechi ya Super Cup ichezwe Saudi Arabia badala ya Hispania.
Jaji mmoja amehitimisha katika uamuzi wake kuwa kuna dalili za mchezo mchafu kwenye mpango huo kati ya Pique na kampuni yake ya Kosmos pamoja na Shirikisho la Soka Hispania (RFEF).
Taarifa ya mahakama hiyo ilifafanua kuwa aliyekuwa rais wa RFEF, Luis Rubiales, kampuni ya michezo ya Sela inayomilikiwa na serikali ya Saudi Arabia pamoja na Pique walisaini makubaliano mwaka 2019.
Katika makubaliano hayo, Kosmos, kampuni inayomilikiwa na Pique ilitakiwa kupewa mgawo wa Euro 40 milioni kwa kufanikisha mechi hizo kufanyikia Saudi Arabia kila mwaka.
“Ukweli ambao unafanyiwa uchunguzi katika sakata hilo unatokana na kuwapo uwezekano wa kikiukwa kwa taratibu kunakohusisha makosa ya kijinai katika makubaliano au mikataba iliyofikiwa,” ilieleza taarifa ya mahakama.
Mahakama imekuwa ikichunguza tuhuma hizo tangu Juni 2022 ikitaka kujua kama Rubiales alihusika na makosa ya jinai katika uongozi wake baada ya RFEF kukubaliana na kampuni ya Kosmos kuhamishia mechi za michuano hiyo Saudi Arabia.
Mwezi Machi mwaka huu, polisi walifanya uchunguzi katika makao makuu ya ofisi za RFEF pamoja na nyumba inayomilikiwa na Rubiales na kukamata watu saba katika sakata zima la uchunguzi wa tuhuma hizo ambapo mamilioni ya Euro yanadaiwa kutumika.
Rubiales ambaye alitajwa kwa mara ya kwanza katika sakata hilo na kuhojiwa na polisi mwezi Aprili, amekana kufanya kosa lolote wakati Pique hadi sasa bado hajasema lolote.
Mtu mwingine anayehusishwa na sakata hilo ni Pedro Rocha ambaye wakati wa matukio hayo alikuwa mkuu wa idara ya uchumi ya RFEF lakini hakuitisha kikao cha kamati ya uchumi kama inavyotakiwa baada ya mkataba wa Kosmos na RFEF kuongezwa miaka mingine minne.
Mwezi uliopita Rocha alichaguliwa kuwa rais wa RFEF licha ya kuwa katika uchunguzi wa sakata hilo baada ya kutoa ushahidi mahakamani akidai kwamba hana chochote anachojua au kuhusika kwa namna yoyote katika makosa ya kijinai anayochunguzwa.
