Manchester, England
Mshambuliaji wa zamani wa Man United, Wayne Rooney amesema kocha Pep Guardiola ambaye hivi karibuni ametangaza kuachana na klabu ya Man City, ni Sir Alex Ferguson wa zama hizi.
Pep amekuwa kocha Man City kwa takriban miaka 10, ametangaza kuachana na timu hiyo baada ya msimu huu akiwa amejipatia mafanikio lukuki ikiwamo kutwaa mataji ya Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya na mengineyo.
Ezi zake akicheza soka la ushindani, Rooney alikuwa mshambuliaji tishio Man United chini ya Ferguson, timu ambayo ameichezea kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.
Ferguson akiwa kocha wa Man United aliweka rekodi ya kubeba mataji 13 ya Ligi Kuu England wakati Pep amebeba taji hilo mara sita.
Rooney bila kujali tofauti hiyo, amesema anauona mfanano baina ya makocha hao na anachoweza kusema ni kwamba Ferguson ndiye bora zaidi lakini Pep kwa kizazi chake naye ni bora.
“Nimesikia watu wakisema kwamba Pep amekuwa muungwana kwa klabu kwa kuiongoza kwa miaka 10 jambo ambalo ni la kipekee lakini Ferguson amefanya hivyo hivyo kwa miaka 26,” alisema Rooney.
Rooney ambaye pia alikuwa mshambuliaji wa timu ya taifa ya England, alisema ukiifikiria miaka mingi namna hiyo, miaka 26 katika klabu moja ya soka hilo ni jambo la kipekee.
Alipoulizwa iwapo Ferguson na Pep walikuwa wakitumia mfumo wa aina moja, Rooney alisema kwamba soka limebadilika kutoka kizazi hadi kizazi pamoja na aina ya uchezaji.
