Na mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay, amesema maboresho yaliyofanyika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, yameipa thamani michuano ya Kombe ka Mapinduzi na mchezo wa soka Visiwani Zanzibar.
Akizungumza leo Jumatatu, Mayay (pichani) alisema miongoni mwa thamani hiyo ni ongezeko la watu walioingia uwanjani kushuhudia mechi za michuano hiyo pamoja ongezeko la zawadi kwa washindi.
“Lazima tuipongeze Serikali kwa maboresho haya, hii itaongeza thamani ya mchezo wa soka Zanzibar lakini hata vijana, makampuni na matajiri mbalimbali watajitokeza kuwekeza kwenye michezo,” alisema Mayay.
Akizungumzia mashindano hayo kwa ujumla, alisema yameendelea kuimarika kila mwaka na kitendo cha waandaji kuongeza zawadi kwa washindi kimeongeza chachu na ushindani kwa timu za Zanzibar na zinazotoka Tanzania Bara.
Kiongozi huyo alitolea mfano mchezo wa fainali uliozikutanisha Mlandege na Simba, watu wengi walikuwa wakiipa nafasi Simba lakini baada ya dakika 90 wenyeji Mlandege waliibuka washindi na hiyo ilitokana na uwekezaji pamoja na miundombinu imara iliyopo visiwani humo kwa sasa.
“Lakini angalia uthubutu na utekelezaji wa majukumu wa wachezaji wa Mlandege, mpira wa miguu unapimwa kwa vita ya katikati ya uwanja, ukiangalia jinsi walivyokuwa wanawakaba washambuliaji wa Simba inaonesha malengo yao yalikuwa nini,” alisema Mayay.