Na mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ ameihimiza klabu ya mpira wa kikapu ya Pazi kujitahidi katika michuano ya Afrika kwa kufanya vizuri ikijua wazi kuwa imebeba jukumu la kitaifa.
Pazi imefuzu kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Kikapu Afrika itakayofanyika Afrika Kusini kuanzia Novemba 14 hadi 19, mwaka huu baada ya kufanya vizuri katika michezo ya Kanda ya Afrika Mashariki hivi karibuni.
“Nilihudhuria katika mashindano hivi karibuni na kuona Pazi inacheza kama timu, niwatie moyo waendelee kufanya hivyo, wafahamu wana bendera ya nchi, na sisi tuna sababu ya kuishabikia kwa sababu ni timu bora,” alisema MwanaFA.
Alisema kinachohitajika kwa sasa ni mashabiki wa kikapu kurudisha mioyo yao katika mchezo huo kwa kujitokeza pindi yanapokuwepo mashindano ili kuwatia hamasa wachezaji.
MwanaFA alisema wao kama serikali wana maagizo kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga viwanja viwili vya ndani Dar es Salaam na Dodoma kwa ajili ya kutoa nafasi ya kuandaa mashindano makubwa.