Na mwandishi wetu
Mwanasheria wa kiungo Feisal Salum au Fei Toto, Jasmin Razak amesema kuwa sasa wako tayari kukutana na Yanga kulimaliza suala la mchezaji huyo baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuziagiza pande hizo kulimaliza suala hilo.
Jasmin amemshukuru Rais Samia kwa kutoa ushauri wa hekima wa kumaliza jambo hilo kwa kuwa hata yeye amekuwa akipambana kulimaliza kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa na haipendezi kwenda kulumbana kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Kimichezo Kimataifa (CAS).
“Imekuja kama mshtukizo lakini nitoe shukrani zangu za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan, mama yetu amelimaliza kwa hekima au ametoa ushauri tulimalize, kitu ambacho nimekuwa nikikipigania siku zote, tulimalize kwa maslahi ya taifa letu.
“Hili sio suala la kwenda CAS, Zurich kulumbana huko, sisi ni Watanzania, tutasikiliza masharti ya Yanga nasi tutazungumza nao, kama binadamu hatuwezi kushindwana na tumeshapewa mwongozo wa Ofisi ya Rais, tutakaa tulizungumze, tulimalize kwa amani,” alisema Jasmin.
Alisema Rais Samia ameingilia kati kwa kuwa anataka kuwatia moyo vijana, sasa haipendezi wao wanaosimamia vijana hao kutokuwa kitu kimoja kwa ajili ya kupelekea mpira wa Tanzania mbele, hivyo wako tayari kwa majadiliano na Yanga.
Hivi karibuni Fei Toto ambaye tangu Desemba, mwaka jana alipeleka barua yake ya kuvunja mkataba na Yanga, aliibuka na kusema anachangisha fedha za kupeleka kesi yake CAS akiamini huko atapata haki yake baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuamua kumrejesha Yanga.
Kwa sasa hata hivyo mambo yanaonekana kupungua makali baada ya Rais Samia kumtaka Rais wa Yanga, Hersi Said kukaa chini na kuumaliza mgogoro huo ambao hauendani na hadhi iliyonayo Yanga kwa sasa.