Na Hassan Kingu
Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC msimu ujao wa 2022/23 imetoka rasmi jana na kama kawaida mechi ya timu pendwa za Yanga na Simba ikitarajia kuchezwa Oktoba 23, mwaka huu.
Hiyo itakuwa ni mechi ya kwanza katika mechi mbili watakazokutana kwenye Ligi Kuu ya NBC ukiachana na ile ya awali ya mechi ya Ngao ya Jamii watakayopepetana Agosti 13, mechi inayoashiria kufunguliwa rasmi kwa pazia la ligi hiyo.
Kwa maana hiyo timu hizo zitakutana mara mbili katika kipindi cha miezi miwili. Kiburudani ni jambo jema na hata kiushindani ni jambo jema kama ambavyo aliwahi kusema aliyekuwa kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo kwamba mechi za watani wa jadi zina umuhimu wake katika maendeleo ya soka lakini inaweza kuwa athari kubwa kwa mabenchi ya ufundi ya timu hizi.
Imezoeleka kuwa mara kadhaa mechi hizi hutoa taswira ya ajira ya makocha wa timu hizi kitu ambacho si kizuri, viongozi wa hizi timu kwa miongo mingi iliyopita wamekuwa wakiwahukumu makocha au vibarua vyao kuanza kutetereka baada ya mechi hizi.
Kiweledi sio jambo jema kwa kocha kuhukumiwa kwa michezo miwili pekee na kutotiliwa mkazo matokeo ya mechi zake nyingine hapa katikati, hukumu hizi ziishie kwa mashabiki tu kama ilivyokuwa kwa kocha mpya wa Simba ambaye baadhi ya mashabiki wa Yanga walishaanza kusema kwamba mwisho wake ni Agosti 13.
Kabla ya kukutana na Simba, Yanga itapepetana na Polisi Tanzania kisha Coastal Union kwa mwezi Agosti kabla ya kuivaa Azam, Mtibwa Sugar na Ihefu kwa mwezi Septemba. Pia mwezi Oktoba itaanza na Ruvu Shooting na Namungo kabla ya kuiingia Simba.
Kimabadiliko ya mazingira na uwekezaji, hizo mechi zote za Yanga kabla ya Simba zina ugumu na mvuto hasa. Ukiangalia usajili wa Azam, Coastal, Mtibwa ni timu zilizojidhatiti dhidi ya vigogo hao lakini ajabu hayataangaliwa matokeo haya na kocha anaweza akajikuta akibebeshwa zigo la mechi moja ya Simba.
Ni kama vile Simba itakavyoanza kunyooshana na Geita Gold, Kagera Sugar, KMC, Tanzania Prisons, Mbeya City, Dodoma Jiji na Singida BS kabla ya Yanga na kisha kuziona mechi hizi ngumu kuwa si lolote isipokuwa ya Yanga pekee.
Usajili wa Geita, Dodoma na hata Singida kwa kutolea mfano si timu za kubeza na ndizo zenye pointi nyingi za kuchangia ubingwa au nafasi ya kushiriki michuano ya klabu Afrika kuliko mechi moja dhidi ya Yanga.
Hizi timu zikiendelea na kasumba ya timuatimua kupitia Kariakoo Derby bado zitakuwa zinajirejesha nyuma licha ya kuwa na mabadiliko ya uendeshaji kwa sasa.
Soka letu la sasa linahitaji uvumilivu na uyakinifu wa maamuzi kwa faida ya ukuaji bora wa timu, hivyo hata baada ya mechi hiyo ya awali ya Watani, tungependa kuona kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi akiendeleza jahazi dhidi ya mechi ngumu zinazofuata za KMC na Geita.
Kama vile tunavyopenda kuona kocha mpya wa Simba, Zoran Maki akipewa nafasi zaidi ya kuona alichonacho dhidi ya Azam iliyojipanga kwelikweli na Mtibwa iliyonusurika kushuka daraja mwisho wa msimu huu.
Baada ya maamuzi mengi yaliyopita ambayo yalitukwamisha kuona ladha ya soka ya namna makocha wanavyobadili mchezo mwisho wa msimu baada ya matokeo ya awali, basi angalau msimu huu pia uanze na mabadiliko kwa hizi timu kama zenyewe zilivyo ‘bize’ kubadili namna ya uendeshaji wa klabu.
Ukiachana na mechi hizo za awali za mapacha hao wa Kariakoo, mechi nyingine zinazotarajia kuwa na mvuto ni ya Azam dhidi ya Kagera itakayopigwa Agosti 17. Mara zote timu hizi zinapokutana huwa hazitabiriki na msimu huu zimajipanga mno, inatarajiwa burudani kali.
Nyingine ni ile ya Agosti 21 ni ya Mtibwa dhidi ya Ruvu, zote zilipitia wakati mgumu msimu uliopita. Ruvu ilihusika kuizamisha Mtibwa kwenye mechi yao ya mwisho kabisa ya msimu ili yenyewe inusurike isicheze ‘play-off’.
Mtibwa imesurika janga hilo na sasa itakutana na hasimu wake mapema tu kwenye ligi hii, ni suala la kusubiri kitakachotokea. Mechi ya Septemba 17 baina ya Namungo na Coastal ni mechi nyingine kali pia kutokana na namna walivyopigana vikumbo msimu uliopita kumaliza kwenye nafasi za juu na sasa kila mmoja amejiimarisha.
Kwa kifupi ni burudani ya kutosha kwa kutazama usajili ulivyofanyika na ratiba ilivyokuwa, kila timu inaonekana moto na kama ushindani huu wa usajili utahamia kama ulivyo kwenye viwanja vya Ligi Kuu ni wazi ligi itaonekana imewahi kuisha kutokana na utamu utakaopatikana ingawa kiuhalisia itachelewa kidogo na kumalizika Juni 10, mwakani.
Soka Miezi miwili ya Dar Derby mbili
Miezi miwili ya Dar Derby mbili
Read also