Na mwandishi wetu
Timu ya TRA United au Watoza Kodi, imetoa kichapo cha mabao 4-1 kwa Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, leo Ijumaa, Mei 8, 2026.
Azam waliuanza mchezo kwa kasi wakionesha dhamira ya kusaka pointi tatu na kasi yao ilizaa matunda mapema dakika ya saba walipopata bao lao pekee lililofungwa na Japhet Kitambala aliyeitumia pasi ya Sadio Kanoute.
Iliwachukua dakika 12 TRA kusawazisha bao hilo mfungaji akiwa Ally Ng’anzi aliyeyatumia vizuri mapungufu ya safu ya ulinzi ya Azam kuipatia TRA bao la kusawazisha kwa pasi ya Ally Mapaka.
Kuingia bao hilo hakukuwasumbua Azam ambao waliendelea kuonesha uhai ingawa kadri muda ulivyokwenda ndivyo kasi ya TRA ilivyoongezeka na Azam kujikuta wakipachikwa mabao mawili ya haraka haraka.
Mabao hayo yalifungwa na Amy Mapaka katika dakika ya 41 na Mapaka tena akaongeza bao la pili dakika ya 44 na kuifanya TRA iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-1.
Karamu ya mabao ya TRA ilikamilishwa dakika ya 64 kwa bao lililofungwa na Ramadhan Chobwedo aliyefumua shuti kali lililomshinda kipa Aishi Manula wa Azam.
Matokeo hayo mbali ya kuvuruga mbio za Azam katika kulisaka taji la ligi hiyo, pia yanakuwa yameivunja rekodi ya Azam ya kutopoteza mechi zake za ligi msimu huu.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa leo, Namungo wakiwa nyumbani Lindi walishindwa kuwadhibiti wageni wao Mashujaa na kujikuta wakitoka sare ya bila kufungana.
Kimataifa Watoza kodi waichapa Azam 4-1
Watoza kodi waichapa Azam 4-1
Read also
